Kushuhudia Mashemeji Derby Sh200 tu

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo na kampuni ya Big Brother Events and Ticketing iliyopewa tenda ya kusimamia viingilio katika mchezo huo, kwa niaba ya timu mwenyeji, ambao ni Ingwe, ili kutizama mechi hiyo mubashara ugani Kasarani, viingilio vya jukwaa kuu vitakuwa ni shilingi 500 huku viingilio vya mzunguko vya kawaida vikipangwa kuwa ni shilingi 200.

Nairobi. Mashabiki wa Gor Mahia na AFC Leopards watashudia mtanange wa kukata na shoka ya Mashemeji Derby kwa shilingi 200 tu Jumapili hii, Julai 22, kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo na kampuni ya Big Brother Events and Ticketing iliyopewa tenda ya kusimamia viingilio katika mchezo huo, kwa niaba ya timu mwenyeji, ambao ni Ingwe, ili kutizama mechi hiyo mubashara ugani Kasarani, viingilio vya jukwaa kuu vitakuwa ni shilingi 500 huku viingilio vya mzunguko vya kawaida vikipangwa kuwa ni shilingi 200.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa tiketi hizo zitapatikana siku ya mtanange kuanzia saa tatu asubuhi, saa chache kabla ya mechi yenyewe itakayotimua vumbi kuanzia saa tisa alasiri.
Hii ni mechi ya tatu inayokutanisha mahasimu hao wa soka la Kenya, msimu huu. Katika mechi mbili za awali, KPL Super Cup na Hull City Challenge, zote zikisakatwa ugani Afraha-Nakuru, Kogalo waliibuka wababe.
Awali kabla ya kuhamishiwa Kasarani, mchezo wa Jumapili, ulikuwa umepangwa kufanyioa mjini Kakamega katika uwanja wa Bukhungu.
Mechi hiyo ililazimika kuahirishwa baada ya Shirikisho la Soka nchini (FKF), kuziomba klabu hizo, kuwaruhusu baadhi ya mastaa wake kujiunga na kambi ya Harambee Stars.
Kuelekea mtanange wa Jumapili, Gor Mahia wanaongoza ligi wakiwa na alama 49, mechi mbili mkononi na tofauti ya pointi tisa kati yao na Sofapaka, inayoshika nafasi ya pili na pointi zake 40. Ingwe wao wako katika nafasi ya tano kwenye jedwali, wakiwa na pointi zao 36.
Kingine ni kwamba, kuelekea mechi hii, Kogalo wanajivunia rekodi nzuri ya kutofungwa hata mechi moja msimu huu, wakiwa wameshinda mechi zao sita za hivi karibuni, licha ya Straika wao matata, Meddie Kagere kutimkia Simba ya Tanzania. AFC Leopards wao wameshinda mechi mbili tu kati ya tano za hivi karibuni.