Azam FC walistahili ubingwa wa Kagame, wengine zindukeni sasa

Muktasari:

  • Klabu hiyo iliyoasisiwa mwanzoni mwa 2000 na kupanda Ligi Kuu Bara 2008 imeweka rekodi ya kutetea taji la michuano hiyo ikifuata nyayo za Simba iliyofanya hivyo 1991 na 1992, 1995 na 1996 kisha Yanga nao kurejea mwaka 2011 na 2012.

KILA mkulima huvuna kile alichopanda. Azam FC walipanda juhudi na maarifa na juzi usiku wamevuna ubingwa wa Kombe la Kagame 2018.

Klabu hiyo iliyoasisiwa mwanzoni mwa 2000 na kupanda Ligi Kuu Bara 2008 imeweka rekodi ya kutetea taji la michuano hiyo ikifuata nyayo za Simba iliyofanya hivyo 1991 na 1992, 1995 na 1996 kisha Yanga nao kurejea mwaka 2011 na 2012.

Haya ni mafanikio makubwa kwa klabu hiyo tajiri na inayoendeshwa kisasa nchini na kwa hakika walistahili ubingwa na Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo hususan soka tunawapongeza kwa mafanikio hayo.

Inawezekana wengi hawajui, ila ukweli, Azam tangu walipofungwa mabao 2-0 na Yanga katika fainali yao ya kwanza ya michuano ya Kagame mwaka 2012 haijawahi kufungwa ndani ya dakika 90 na timu yoyote hadi mwaka 2018.

Mwaka 2014 iliondolewa kwenye robo fainali ya michuano iliyofanyika mjini Kigali, Rwanda kwa mikwaju ya penalti baada ya kumaliza dakika 90 bila kufunga na tangu hapo imeshiriki michuano hiyo misimu miwili mfululizo bila kupoteza.

Mwaka 2015 walipochukua taji lao la kwanza la Kagame waliweka rekodi ya kutoruhusu bao hata moja na safari hii wamelitetea tena bila kupoteza mchezo wowote kama ilivyokuwa katika msimu wa mwisho wa mashindano hayo 2015.

Haya sio mafanikio madogo hata kidogo kwa klabu hiyo, ikizingatiwa imekutana katika ushiriki wake wote wa misimu mitatu ya michuano hiyo, imekutana na klabu zoefu za michuano hiyo, lakini zote imefanikiwa kuzimudu.

Azam katika Kagame 2015 ilivaana na KCCA ya Uganda, Yanga, Gor Mahia ya Kenya waliowafunga fainali na kurejea tena kuwanyoosha kwenye mechi ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu kabla ya kuivaa Simba wenye rekodi ya kubeba taji hilo mara nyingi kuliko timu yoyote za Afrika Mashariki na Kati.

Simba imelitwaa taji hilo mara sita katika fainali 12 ilizofanikiwa kucheza, kwa maana juzi ilikuwa fainali yake ya sita kupoteza katika michuano ya Kagame.

Ndio maana tunasisitiza kwa hakika Azam walistahili kubeba taji kwa vile ilionyesha mapema haikushiriki tu, bali iliingia Kagame kupambana na imefanikiwa.

Pamoja na ukweli katika soka kuna kushinda na kushindwa, lakini matokeo ya timu hiyo kufanikiwa kutetea taji hilo kwa mara ya pili mfululizo ni kuonyesha namna gani Azam walivyo makini inapokuja michuano ya kimataifa.

Azam iliingia kwenye Kagame ikiwa imedhamiria kutetea taji na tangu mchezo wao wa kwanza wa makundi walionyesha dhamira hiyo na wameendelea nayo mpaka kufika fainali na hatimaye kutwaa taji hilo kwa mara ya pili.

Tunaamini timu zetu zikiwa zinaingia kwenye mashindano ya kimataifa zikiwa na dhamira ya ushindi na wachezaji kujituma mwanzo mwisho katika mechi zao kama ilivyofanya Azam.

Tunafahamu hata Simba walistahili pongezi hizi kwa kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu warejee kwenye michuano hiyo waliyoishiriki mara ya mwisho mwaka 2012 na kufungwa mabao 3-1 na Azam katika robo fainali.

Kwani kutinga kwao hatua hiyo ya fainali sambamba na Azam walilifanya taji hilo libakie katika ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine, lakini bado Azam wanastahili pongezi zaidi kwa kuweza kuwashinda kwa mara nyingine na kutetea taji lao.

Hata hivyo, mafanikio ya Azam yawe chachu kwa klabu zetu zinazoiwakilisha nchi, kuanzia Yanga waliopo makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mpaka Simba na Mtibwa Sugar zitakazoiwakilisha nchini mwakani katika michuano ya CAF.

Lazima ziingie kwenye michezo ya michuano hiyo ya Afrika kwa nia moja tu ya kufanya kweli kwa kupata matokeo ili kuendelea kupeperusha bendera ya nchini.

Yanga Jumatano ijayo itakuwa Kenya kuvaana na Gor Mahia katika mechi ya Kundi D la michuano ya Shirikisho Afrika, iende Nairobi ikitambua ina kazi kubwa ya kufanya kuweza kuibeba Tanzania mbele ya Wakenya.

Imefika wakati sasa klabu za Tanzania kuondoa unyonge mbele ya timu za mataifa mengine ya Afrika kwa kupata matokea mazuri bila kujali zinacheza nyumbani ama ugenini, unyonge ambao kwa hakika tunaona ndio kigezo cha kufanya vizuri kimataifa.

Ndio maana tunazitaka klabu zetu kujifunza kupitia mafanikio ya Azam katika michuano ya Kombe la Kagame, ili kuthibitisha Tanzania ya sasa imeondoka na ule usemi wa kuwa, Kichwa cha Mwendawazimu.