Sintoshangaa sana Croatia wakibeba ndoo huko Moscow

Muktasari:

  • Leo Jumapili inapigwa mechi ya 64 ya michuano hiyo kuhitimisha pilikapilika za siku 31 za fainali hizo zilizoshuhudiwa jumla ya mabao 161 yakifungwa katika mechi 62 (kabla ya mchezo wa jana Jumamosi wa kusaka mshindi wa tatu).

HAKUNA utabiri wowote mwingine tena kwa sasa. Jioni ya leo Jumapili Bingwa Mpya wa Kombe la Dunia 2018 lazima awe ama Croatia au Ufaransa basi!

Hao ndio wanaume waliohimili vita na vishindo vya mwezi mmoja wa fainali hizo zilizofanyikia Russia tangu Juni 14.

Leo Jumapili inapigwa mechi ya 64 ya michuano hiyo kuhitimisha pilikapilika za siku 31 za fainali hizo zilizoshuhudiwa jumla ya mabao 161 yakifungwa katika mechi 62 (kabla ya mchezo wa jana Jumamosi wa kusaka mshindi wa tatu).

Kabla na hata baada ya kuanza kwa michuano hiyo, kulikuwa na tabiri nyingi na chambuzi zilizozipigia chapuo baadhi ya timu kuwa, lazima zifike mbali na hata kubeba taji hilo. Wengine walikidiri hata kutabiri wale watakaonyakua Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora, turufu zikiwaangukia baadhi ya mastaa wakubwa. Waliokuwa watetezi, Ujerumani, Mexico, England, Argentina, Ureno, Ubelgiji, Brazili, Ufaransa, Hispania na Senegal kwa nchi za Afrika zilipigiwa chapuo msimu huu zikipewa nafasi kubwa ya kutamba Russia. Wapo waliodiriki hata kubeti na kuweka mzigo kwa timu hizo wakiamini zitafika mbali na hata kubeba taji hilo. Ni wachache tu waliothubutu kuweka mzigo kwa Ufaransa labda ndio kwa sasa wanatabasamu, lakini wengine wamechana mikeka.

Hii ni kwa sababu michuano ya mwaka huu ilikuwa na matokeo ya kustaajabisha.

Kama kuna timu haikupewa nafasi kabisa kung’ara Russia, lakini ikafanya maajabu basi ni Croatia. Hii ndio timu iliyoshangaza wengi, pia imeandika rekodi ya kuwa timu pekee iliyocheza dakika nyingi zaidi katika fainali za 2018.

Ndio, kama hujui, kabla ya mchezo wa leo, Croatia imecheza dakika 90 zaidi kuliko timu yoyote ikiwamo wanafainali wenzao Ufaransa.

Kuanzia hatua ya 16 walipovaana na Denmark, kisha kucheza na wenyeji Russia katika robo fainali kabla ya kuwatoa nishai England katika nusu fainali, Croatia mechi hizo zote ilikuwa ikitumia dakika 120 kuweza kupata matokeo yake.

Ukichukua dakika 30 za nyongeza za pambano lao la Denmark na ukijumlisha na zile nyingine za mechi zao na Russia na England utapata jumla ya dakika 90 ikiwa ni sawa na timu hiyo kucheza mchezo mmoja wa ziada kabla ya fainali ya leo.

Kupenya kwa Croatia kutoka mechi ya makundi mpaka kufika fainali ilikuwa ni kama miujiza tu, kwani hakuna aliyeitabiria mafanikio hayo. Wengi walisahau kuwa soka ni mchezo wa maajabu na huwa na matokeo ya kustaajabisha kwelikweli.

Sitashtushwa sana kama jioni ya leo Watoto wa Madam hao wakitawazwa Mabingwa wa Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yao, hata kama ni kweli inakutana na Ufaransa iliyokamilika na yenye mapumziko ya ziada kuliko wao. Croatia wanacheza jihadi, hawakati tamaa kirahisi na pia ni wavumilivu na wanaojua kucheza na akili ya wapinzani wao. Fuatilia mechi zao zote walizocheza utabaini hilo.

Ukweli ndivyo ulivyo, Ufaransa imepata mapumziko zaidi kuliko Croatia, kwa vile The Blues walitangulia kucheza mechi yao na nusu fainali Jumanne ndipo siku inayofuata The Blazers a.k.a Vatreni wakamaliza kazi mbele ya Three Lions. Kwa kuangalia jinsi vijana wa Croatia walivyochoshwa katika safari yao ya kufika fainali na muda wa kupumzika iliyopata Ufaransa ni rahisi kuamini The Blues watabeba ndoo mjini Moscow, lakini maajabu ya soka yananikatili kuamini hivyo.

Sitashangaa kuona Luca Modric akinyanyua kwapa jioni ya leo mara baada ya kukabidhiwa taji wakihitimisha kazi waliyotumwa mbele ya Ufaransa ya akina Antonio Greizmann, Paul Pogba na wakali wengine wanaotetemesha duniani.

Naweza kusema tu, Ufaransa itapindua meza tu, kama itaamua kumaliza mchezo ndani ya dakika 90, vinginevyo wakienda muda wa nyongeza itaumizwa kwa vile wapinzani wao wa Croatia ni kama wameshalizoea gwaride la dakika 120. Hivyo wakienda muda wa nyongeza huenda wakapata tabu sana! Hata hivyo, timu yoyote itakayobeba taji hilo katika mchezo wa fainali hiyo ya leo ambayo ni ya 21 ndani ya miaka 88 tangu michuano hiyo iasisiwe mwaka 1930, ni haki yake kwa vile zote zinastahili kwani zimethibitisha kuwa wao ni vidume.

Haikuwa kazi rahisi kwa timu hizo kufika fainali kutokana na ukweli fainali za mwaka huu zilikuwa ngumu na zisizotabirika ndio maana watetezi Ujerumani waliondoka mapema. Lionel Messi na hasimu wake, Cristiano Ronaldo sambamba na bishoo, Neymar wa Brazili walishindwa kuhimili vita hivi ndio maana walitolewa mapema na timu zao pale Russia.

Mastaa hao awali kupigiwa chapuo wangefunika kinoma, lakini kwa kuwa soka ni mchezo wa hadharani, nyota hao walichemsha na huenda leo watakuwa katika sebuleni zao kuangalia vidume wenzao wakitoana jasho mjini Moscow na pengine wakajikuta wakimpigia makofi Modric ama Hugo Lloris watakabidhiwa rasmi taji.