Karia na wenzako jiandaeni kubeba lawama

Muktasari:

  • Tena wote wakiruhusiwa kucheza katika mchezo mmoja kutegemea na uamuzi wa kocha wa timu husika. Huenda wameona kuna umuhimu wa kufanya hivyo kama walivyojitetea mbele ya wanahabari ni kuifanya ligi isisimue na kuvutia wadhamini. Labda?

HAKUNA anayejua kitu gani kilichowafanya mabosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitisha kanuni ya mabadiliko ya idadi ya nyota wa kigeni katika klabu za Ligi Kuu Bara kutoka saba iliyokuwa awali hadi kufikia 10. Tena wote wakiruhusiwa kucheza katika mchezo mmoja kutegemea na uamuzi wa kocha wa timu husika. Huenda wameona kuna umuhimu wa kufanya hivyo kama walivyojitetea mbele ya wanahabari ni kuifanya ligi isisimue na kuvutia wadhamini. Labda?

Ila nawakumbusha mapema mabosi wao, hasa Rais Wallace Karia na Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidau, wajiandae kubeba mzigo wa lawama mbele ya safari, kama Tanzania itashindwa kufanya la maana katika soka la kimataifa. Binafsi sioni tatizo juu ya ongezeko hilo, kwa vile hata DR Congo tumeona haina ukomo wa idadi ya nyota wa kigeni, lakini timu zake za taifa hasa ya wachezaji wa ndani inatisha kila inaposhiriki CHAN, kadhalika klabu zake zinatetemesha Afrika.

Hata hivyo inawezekana wengi hatujui nyuma ya mafanikio ya timu za DR Congo! Wachezaji wa Kongo wanajitambua, wana kiu ya maendeleo na wapo tayari kupambana kwa ajili ya kupata namba ndani ya timu zao za taifa. Wachezaji wetu wana silka hiyo ya kupambana? Je wameandaliwa kukabiliana na ongezeko hilo, ama mabosi wa TFF na washirika wao walioshinikizana kuongeza idadi wamejipanga vipi kuwasaidia nyota hao kukabiliana na changamoto iliyopo mbele juu ya ongezeko la mapro wa kigeni? Nakumbuka Agosti, 2014 aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla aliwahi kutoa ushauri kutaka idadi ya nyota wa kigeni iliyokuwapo wakati huo ya wachezaji watano ipunguzwe kwa kuhofia kuzimika kwa vipaji vya wazawa.

Kama wachezaji watano walimtisha Dk Msolla, lakini uongozi wa kina Jamal Malinzi ukaamua kuongeza wawili wa ziada ambao umeshindwa kuleta tija wala kuwaamsha wachezaji wazawa, vipi hao 10? Bila shaka kuna kiama cha soka mbeleni, ila ngoja tuone hali itakavyokuwa.

Kama mambo yataenda kombo , basi Karia na wenzake wajiandae tu kubebeshwa lawama, kwani Watanzania hasa mashabiki wa soka nawafahamu walivyo vigeugeu, leo wanashangilia kesho watawapopoa mayai!