Hii tozo ya Sh5 milioni! Basata wanajiongopea

Muktasari:

  • Nimeona pia mjadala wa tozo ya Sh5 milioni ambayo msanii atatakiwa kulipiwa ili atumike kwenye matangazo ya biashara.

NIMESOMA kanuni mpya za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambazo zimeweka tozo mpya kwa huduma mbalimbali za sanaa na wasanii nchini. Nimeona pia mjadala wa tozo ya Sh5 milioni ambayo msanii atatakiwa kulipiwa ili atumike kwenye matangazo ya biashara.

Pamoja na kila hoja, ukweli upo wazi Basata wanajiongopea sana. Ipo dhahiri kanuni zao hawakuzifanyia kazi inavyotakiwa. Hawajafanya utafiti kujua msanii anapataje kazi za matangazo na anafaidikaje. Tozo ya Sh5 milioni uamuzi uliotokana na hisia pamoja na fununu.

Hisia kwa maana baraza linahisi wasanii wanafaidika mno. Fununu kwa tafsiri ya kukusanya maneno mitaani na kuona yanatosha kuyaundia kanuni. Mwisho ndiyo uamuzi unatoka kila msanii ili atumike kwenye tangazo la biashara inabidi alipiwe Sh5 milioni.

Kwa uamuzi ambao Basata wameutoa, inaonekana ama hawajui hali halisi za wasanii (hawakufanya utafiti) au kusudi ya maangamizi kwa sanaa ya Tanzania. Safari ambayo Basata na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wameianzisha ni kuipeleka sanaa kuwa sio tena jukwaa la vijana maskini kujiajiri na kujikomboa kimaisha.

Basata na wizara yenye dhamana ya usimamizi wa sanaa, wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha sanaa inakua. Uhakikisho huo wa ukuzaji sanaa lazima uende sambamba na kutengeneza mazingira rahisi ya ufanyaji shughuli za sanaa. Sio kukimbilia kunufaika kupitia wasanii pasipo kujenga misingi.

Basata na Wizara ya Habari sharti kujiweka mbali na mipango ya kutaka kunufaika mahali ambapo hawajapawekea mfumo mzuri. Unaweka tozo kwamba msanii ili atumike kwa tangazo lazima alipiwe Basata Sh5 milioni, wakati huohuo hujaweka bei ya msanii.

Tozo ya Sh5 milioni, Basata wamejifikiria wenyewe lakini hawakuwaweka mawazoni wasanii. Basata wanashindwa kung’amua wao bila wasanii ni baraza lisilo la shughuli ya kufanya. Kwa mantiki hiyo ni vyema kubembelezana na wasanii ili wawepo kusudi na baraza nalo liendelee kutimiza uhalali wa kuwepo kwake.

IPO SHIDA KUBWA

Kuna shida inaonekana hivi sasa ya kutaka taasisi za umma zijiendeshe kibiashara. Matokeo yake ndiyo haya ya Basata kuibuka na tozo nyingi mpaka nyingine zinaonekana kuvuka mipaka. Basata wanatakiwa kubaki kuwa baraza la usimamizi na ukuzaji wa sanaa. Makusanyo ya mapato waachiwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Inavyotokea sasa hivi ni biashara moja kuwa na tozo nyingi. Kama una biashara yako, ikiwa umeamua kutenga Sh30 milioni kwa ajili ya matangazo, ukimgusa msanii fedha hiyo haitatosha.

Basata watataka chao Sh5 milioni, TRA watakuja na makato yao asilimia 18, bado hujamlipa msanii na hujalipia matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari ambako nako kodi italipwa.

Msanii anapopokea malipo ya kibiashara TRA wanapokea kodi na matangazo yakirushwa redioni, kwenye televisheni au magazetini, pia TRA wanachukua kodi. Mwenye biashara yake anapoona sasa kumlipa msanii amtangazie atatakiwa pia kuwalipa Basata Sh5 milioni, hapo atarudi nyuma. Atakimbia.

Hakuna mfanyabiashara mwenye kupiga hesabu ya kutumia kuliko kuingiza. Ndiyo maana hata wasanii wenyewe hawaandiki bei, isipokuwa hufanya makubaliano kwa kuzingatia thamani ya biashara yenye kutangazwa, muda wa mzunguko wa tangazo na hadhi ya msanii husika.

Angalau Basata wangeweka tozo ya asilimia. Mfano msanii anapotumika kwenye tangazo la biashara, asilimia tano ya fedha za malipo ya msanii zinapaswa kulipwa Basata. Kuweka Sh5 milioni ni sawa na kuamini bei ya kila msanii kwenye tangazo ni fedha nyingi na ni sawa, wakati wapo wasanii wengi hawajawahi kuonja hata Sh100 ya tangazo.

Mtangazaji wa biashara anapoingia makubaliano na msanii kwa ajili ya kufanya tangazo, gharama ni nyingi. Kulipia mandhari ya kurekodi, mavazi, inapobidi malazi, usafiri na kila kitu kitu chenye kutumika kufanikisha tangazo husika hulipiwa kodi TRA. Unaongeza na Sh5 milioni. Si kingine unachokitafuta zaidi ya kutaka wasanii wakimbiwe.

FUNUNU NA HISIA

Nimeeleza hapo awali kuwa Basata wameweka tozo ya Sh5 milioni kwa fununu na hisia. Hapa naomba nifafanue. Basata wanaona wao kama walezi wa wasanii, kuna wasanii wanatengeneza fedha nyingi kupitia sanaa halafu wenyewe hawanufaiki moja kwa moja na mnyororo huo wa mapato.

Basata wanasahau au wanashindwa kuelewa fedha ambazo TRA wanakusanya ni mapato ambayo Basata wanahusika nayo moja kwa moja. Sanaa haiwezi kukuzwa kwa nyongeza nyingi za tozo za mapato, bali ni kwenda kuidumaza. Hili linapaswa kuzingatiwa na Basata.

Ni uamuzi wa fununu na hisia kwa sababu mathalan, ipo minong’ono Diamond Platnumz hulipwa fedha nyingi za mkataba wa matangazo. Ni rahisi pia kupatia ukisema ukimtaka Ali Kiba au Vanessa Mdee kwa ajili ya tangazo inabidi uandae kitita cha nguvu, vinginevyo huwezi kupata huduma yao.

Wakati fulani ilivuja kwenye vyombo vya habari kuwa mkataba wa matangazo kati ya Diamond na Vodacom ulifikia Sh750 milioni. Basata wanapoona tarakimu kama hizo wanashtuka. Iwe kwa ukweli au kujiridhisha kwao, wanapaswa kufahamu hao ni Diamond na Vodacom.

Thamani ya Diamond ipo juu sana. Vodacom ni kampuni kubwa ya kibiashara. Inawezekana wakati wowote tangazo la biashara kati ya Diamond na Vodacom lisiathiriwe na tozo ya Sh5 milioni. Hata hivyo, si kila msanii ni Diamond. Vipi mwenye duka lake la nguo, akitaka kufanya tangazo na Ally Nipishe wa THT? Hiyo milioni 5 itapatikanaje?

Wasanii ni wengi na biashara ni nyingi. Zipo kubwa, za kati na ndogo. Kila kundi lingependa kupata huduma ya matangazo. Tozo ya Sh5 milioni itayaathiri makundi ya wafanyabiashara wadogo na kati, kisha wasanii wadogo na hata wakubwa wenye nguvu ndogo kibiashara watakosa ulaji.

USHAURI WA JUMLA

Ushauri unakwenda moja kwa moja kwenye wizara yenye dhamana ya sanaa. Iache kuzisukuma idara zake ambazo ni taasisi za umma ili zijiendeshe kibiashara. Sanaa inalipa kodi TRA, hivyo ni wajibu wa Serikali kupitia Hazina, kuendelea kuwapa ruzuku ya kutosha Basata na hata Bodi ya Filamu.

Basata, Bodi ya Filamu na taasisi nyingine za sanaa, ziachwe zitekeleze majukumu ya usimamizi wa maudhui, misingi na ukuzaji wa sanaa kwa jumla. Kutaka zijitegemee au zijiendeshe kibiashara, ndipo hapo tunakutana na tozo ambazo zinatengeneza alama nyingi za mshangao. Katika kanuni mpya za Basata, msanii anayetoka nje ya nchi lakini ndani ya Afrika Mashariki anatakiwa kulipiwa kibali chenye thamani ya Sh1 milioni na endapo atakuwa anaingia nchini kwa dhararu kibali chake ni Sh2.5 milioni. Basata wameshindwa kutambua kuhusu uwepo wa nguzo saba za Soko la Pamoja Afrika Mashariki.

Nguzo hizo saba za Soko la Pamoja ni usafirishaji na uhamaji huria wa bidhaa, huduma, mitaji, uhamaji huru wa watu, wafanyakazi, haki kuweka maskani na makazi. Kama taasisi ya umma yenye kuheshimu mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, haipendezi kuona mwaka 2018 bado msanii wa Afrika Mashariki anatozwa Sh2.5 milioni kuingia nchini kufanya kazi.

Upande wa Bodi ya Filamu malalamiko ni mengi mno. Msanii akitaka kurekodi filamu au tamthiliya apeleke kwanza muswada ukaguliwe, hapo anatozwa Sh500,000. Baada ya hapo anapewa kibali cha kwenda kurekodi.

Filamu au tamthiliya ikisharekodiwa, inarudishwa tena bodi ili ikaguliwe na kila dakika inatozwa Sh1,000.

Filamu au hiyo hiyo tamthiliya ikiingia kwenye mzunguko wa biashara, TRA wapo kuchukua makato yao. Je, lengo ni kuua sanaa?

Maisha yenyewe kama haya, badala ya kulegeza mazingira ndiyo kwanza yanakazwa. Mapato yaachwe TRA wayakusanye. Kwingine kama Basata, Bodi ya Filamu na kadhalika, waachwe watoe huduma za ukuzaji sanaa.