England yawaaga Vardy, Cahill, Young

Muktasari:

Hata hivyo wakati England ikilazimishwa kusubiri hadi 2022 kujaribu tena bahati yao katika kuliwania Kombe la Dunia, bila shaka sehemu kubwa ya wachezaji walioifikisha hapo hawatakuwepo kutokana na umri kuwatupa mikono.

Moscow, Russia. Ndoto za England kutinga fainali ya Kombe la Dunia, imezimwa na Croatia, baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa juzi.

Hata hivyo wakati England ikilazimishwa kusubiri hadi 2022 kujaribu tena bahati yao katika kuliwania Kombe la Dunia, bila shaka sehemu kubwa ya wachezaji walioifikisha hapo hawatakuwepo kutokana na umri kuwatupa mikono.

Wachezaji hao wenye umri wa zaidi ya miaka 30 na ambao kuna uwezekano mdogo wa kuendelea kuwepo dimbani katika fainali zijazo za Kombe la Dunia ni pamoja na Ashley Young, Jamie Vardy, Gary Cahil, Phil Foden, Ryan Sessegnon, Lewis Cook na wengine kadhaa.

Kuna wasiwasi kwamba wachezaji hao wanaweza wasiwepo hata katika kikosi cha England kitakachoriki fainali zijazo za mataifa ya Ulaya ‘Euro 2020’

Bilas haka Kocha wa England, Gareth Southgate, atalazimika kutimiza mpango alioudokeza hivi karibuni kwamba anapaswa kusuka kikosi kitakachoundwa na damu changa kwa kiasi kikubwa ili kujiandaa na Euro 2020.

Tayari Kocha huyo ameanza kurushiwa vijembe na baadhi ya wadau wa soka wakimwambia ‘vibabu’ wachezaji hao wenye umri mkubwa ndio waliomuangusha mbele ya Croatia licha ya kupambana na kufika nusu fainali.

Hata hivyo Kocha Gareth Southgate, amewapuuza wanaomkosoa akisema kikosi chake kwa kiasi kikubwa kiliwategemea vijana akiwemo nahodha wa kikosi hicho Harry Kane, ambaye ndiyo kwanza anaanza kuchanua katika ulimwengu wa soka.