Usajili wa Ronaldo Juventus, Wafanyakazi Fiat wagoma

Milan, Italia. Wafanyakazi wa Kampuni ya utengenezaji magari ya Fiat Chrysler nchini Italia wamekerwa na kitendo cha mmiliki mwenye hisa nyingi ndani ya kampuni hiyo kuamua kutoa Eiro 112 milioni sawa na Pauni 99.2 milioni kumsajili Cristiano Ronaldo kwenda Juventus.

Manung’uniko hayo hayajatolewa na wafanyakazi wa Kampuni hiyo ya magari pekee bali hata walio ndani ya klabu ya Juventus wamepinga matumizi ya fedha hizo nyingi kwa ajili ya mchezaji mmoja.

Wamemnyooshea kidole mwenyekiti wa klabu hiyo bilionea kijana Andrea Agnelli, ambaye pia ndiye mwenye sauti katika Kampuni hiyo ya magari.

“Ni jambo lisilokubalika kwa mtu kuamua kuweka rehani ajira za maelfu ya watu kwa ajili ya mtu mmoja, hili sio sahihi hakukua na sababu za kumsajili Ronaldo mwenye miaka 33 kwa fedha nyingi kiasi hiki,” walinung’unika.

Wamekerwa na uamuzi wa kumsajili Ronaldo kutoka Real Madrid kwa mkataba wa miaka minne ulioigharimu klabu hiyo Pauni 99 milioni ambazo inaaminika zinatoka mfuko mwa bilionea huyo, ambazo bila shaka zitakua sehemu ya mtaji wa Kampuni hiyo ya magari ambayo imeanza kuyumba kwa karibu miaka miwili sasa.

Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa biashara na uchumi wanamuunga mkono mfanyabiashara huyo wakidai Ronaldo atawalipa.

Mtaalamu wa fedha kwenye soka, Rob Wilson, kutoka Sheffield Hallam University, amesema hana wasiwasi kuwa  Juventus itarudha fedha za kumnunua Ronaldo ndani ya mda mfupi na anaamini klabu hiyo itakusanya fedha nyingi kutokana na kumsajili mshambuliaji huyo nyota duniani.

“Biashara inaonyesha kuwa Juventus wamelamba bingo kwa usajili huu, watavuna kiasi kikubwa cha fedha lakini pia uwanjani Ronaldo atawasaidia sana hasa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya nadhani watapata faida mara dufu,” alisema Wilson.