Katwila: Mtibwa akili yote mashindano ya CAF

Arusha. Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema wachezaji wake wamerudi kambini kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katwila amesema timu yake imeingia kambini tangu Jumatatu kujiandaa na mashindano Afrikapamoja na Ligi Kuu Bara.

“Hadi sasa wachezaji wetu ni wale wale wa kikosi kilichotupatia ubingwa wa Kombe la FA ila hadi wiki ijayo tutajua yupi ataondoka na yupi atabaki ndio tutaanza kuwasaka wachezaji wa kujaza nafasi zao, lakini hadi sasa timu yangu ni ile ile,” alisema Katwila

Alisema wachezaji wa Mtibwa waliokuwepo msimu uliopita bado ni wazuri na watawaongeza wachache kutoka kikosi cha vijana kuwapandisha hivyo watakaowachukua kutoka nje ni wachache sana.

“Siwezi kukutajia yupi ataondoka na yupi atabaki kikubwa watakaomaliza mikataba yao na kulazimika kuachana na sisi ndio tutajaza nafasi zao kwa sasa tambua tu kuwa wachezaji karibia wote bado wana moyo na nia ya kubakia kuhudumia Mtibwa.”

 

Uongozi wa klabu hiyo uko jijini Dar es Salaam kumalizana na Shirikisho la Soka nchini (TFF) juu ya utata wake wa malipo ya dola 1500 kama adhabu ya CAF  kutokana na kushindwa kupeleka timu Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo dhidi ya Santos.

Awali katibu wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur alisema kuwa walishalipa fedha hiyo, lakini uongozi mpya wa TFF wanadai hawana kumbukumbu hiyo hivyo wameamua kwenda Dar-es-salaam kumaliza utata wa adhabu hiyo.