Kariakoo Kagere, Mbagara Morris we acha tu

Muktasari:

Mshambuliaji mpya wa Simba, Kagere amehamishia makali yake ya Gor Mahia wa Kenya katika klabu yake mpya na tayari amefunga mabao matatu katika mashindano Kombe la Kagame, hivyo anatazamwa kuibeba timu yake katika fainali hizo, kutokana na namna anavyotumia nguvu kulazimisha mashambulizi.

Dar es Salaam. Dakika 90 za fainali la Kombe la Kagame, kati ya Simba na Azam FC, kesho Ijumaa kutashudia ufundi, akili, nguvu na kila aina ya mbinu wakati mshambuliaji mahiri Meddie Kagere atakapokutana uso kwa uso na beki kisiki Aggrey Morris kwenye Uwanja wa Taifajijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji mpya wa Simba, Kagere amehamishia makali yake ya Gor Mahia wa Kenya katika klabu yake mpya na tayari amefunga mabao matatu katika mashindano Kombe la Kagame, hivyo anatazamwa kuibeba timu yake katika fainali hizo, kutokana na namna anavyotumia nguvu kulazimisha mashambulizi.

Wakati Kagere akitazamiwa na mashabiki wake kuwatoa kimasomaso, lakini upande wa pili Azam FC yupo beki kisiki, Morris anayeweza akavuruga mipango ya staa huyo.

Aggrey ni kati ya mabeki ambao wanaogopwa katika Ligi Kuu kutokana na jinsi ambavyo wanakuwa wanakamia katika mechi, hivyo wengi wanataraji kuona kama ataweza kumzuia Kagere katika mchezo huo.

Kagere naye atataka kuendeleza ubabe wa kutupia kwani katika Kombe la Kagame amekuwa na upepo mzuri kwenye kutupia, hivyo wengi wanasubili kuona kama atatamba mbele ya Azam au mambo yatakuwa ndivyo sivyo.

Kaimu kocha mkuu wa Simba, Djuma Masoud amesema Azam FC imekamilika kila idara, hivyo haitakuwa mechi ya kitoto.

 

"Azam FC ina mabeki imara, ipo vizuri eneo la kati na ushambuliaji, lakini kikosi changu pia kipo hivyo hivyo hilo litafanya mchezo uwe mgumu zaidi na mwenye kutumia mbinu vizuri ndiye atafanikiwa," alisema Djuma.

Ukiacha vita hiyo mashabiki wa soka watapata nafasi ya kuona ufundi mwingine kutoka kwa nyota wapya wa timu hizo wakionyeshana kazi katika mchezo huo.

BUKABA VS NCHIMBI

Wote hawa ni wachezaji wanahitaji uhakika katika vikosi vyao kwahiyo wanataka kuonyesha kiwango na hakuna ambaye atakubali kirahisi kuonekana ndivyo sivyo katika mechi hii ambayo inasubiliwa kwa hamu.

Bukaba amepata nafasi ya kuanza mfululizo kwenye Kagame baada ya awali kukosa nafasi katika Ligi Kuu, hivyo anataka azidi kufanya vizuri ili kujihakikishia namba kwa kuonyesha utofauti na waliocheza Ligi Kuu.

Wakati huo huo Ditram Nchimbi ambaye bao lake dhidi ya Gor Mahia ndio limewavusha Azam kuingia nusu fainali, anataka kuonyesha kwamba mabosi hao hawakufanya makosa kuchukua uamuzi wa kumsajili.

Litakuwa bato kubwa sana kwao kwani Nchimbi anajua kwamba macho yote yatakuwa upande wake baada ya mshambuliaji Shaban Chilunda kukatazwa na klabu yake mpya kuendelea na mashindano hayo.

MUDATHIR VS KOTEI

Katika sehemu ya kiungo kutakuwa na changamoto kubwa kwa pande zote mbili kutokana na timu zote wana viungo ambao wamekamilika vilivyo.

Mashabiki wanatarajia kuona kivumbi kikubwa katika nafasi hiyo kutokana na umahiri wa pande zote mbili, huku upande wa Azam ambao wanachezesha viungo watatu Mudathir Yahya, Frank Domayo na Salum Aboubakari wameonekana kuelewana sana katika michezo waliyocheza.

Huku kwa upande wa Simba nao wana viungo wazuri, James Kotei, Mzamiru Yassin na Mwinyi Kazimoto, wote wamekuwa wakicheza kwa kukaba vizuri lakini pia kwa kushambulia kwa pamoja.

Kwa aina hii ya viungo tutegemee kuona katika eneo la katikati kutimua vumbi vilivyo kwasababu eneo hilo ndio mashambulizi yanapoanzia katika timu yoyote kwa kutengeneza nafasi.