Mbappe: Sina shida na Ballon d'Or, nataka Kombe la Dunia

Moscow, Russia. Baada ya kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Dunia, wakiitandika Ubelgiji 1-0, kwa goli la kichwa, lililowekwa wavuni na beki wa Barcelona, Samuel Umtiti,  dakika ya 51. Winga wa PSG, Kylian Mbappe, ambaye amekuwa na fomu nzuri kwenye michuano hii, amesema hana mpango na tuzo ya Ballon d'Or.

Mbappe amekuwa mchezaji muhimu kwa Les Blues. Itakumbukwa kuwa aliongoza kuwaua Argentina na hata mchezo wa jana alisumbua sana. Katika michuano hii, kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, pia ameweka rekodi mbili tofauti, ya kwanza ikiwa ni kuvunja rekodi mchezaji kinda kuwahi kufunga bao iliyowekwa na David Trezegeut miaka 20 iliyopita.

Pili ni kufunga mabao mawili katika mchezo mmoja na kuvunja rekodi ya mchezaji kinda aliyewahi kufunga mabao mawili katika mechi moja ya Kombe la Dunia, iliyodumu kwa zaidi ya miaka 60. Rekodi hii iliwekwa na mchawi wa soka, Mbrazil Pele.

Akizungumza na waandishi baada ya kumalizika kwa mechi ya nusu fainali ya kwanza, iliyopigwa jana, Mbappe alisema kwa sasa akili yake inawaza kitu kimoja tu, kuipatia Ufaransa Kombe la Dunia baada yanmiaka ishirini ya kusubiri na wala sio kuanza kuwaza tuzo ya Ballon d'Or akisisitiza kuwa tuzo hiyo itakuja tu muda wake ukifika.

"Siamini, hii ni ndoto kwa kweli. Tangu tunaanza michuano hii tulikuwa na ndoto ya kufika hapa, kilichobaki sasa ni kufanya kitu Julai 15, tutapambana kuweka heshima pale Luzhniki. Watu wameanza kuzungumza kuhusu Ballon d'Or, mimi nitoeni huko, wala hata siifikirii kwa sasa, nawaza Kombe la Dunia tu," alisema Mbappe.

Ushindi waliopata umewapa tiketi ya kuelekea Luzhniki, ambako wanasubiri mshindi kati ya England na Croatia, wanaoumana leo katika uwanja huo wa Luzhniki, katika mchezo wa nusu fainali ya pili. England wanaingia katika mechi hiyo, wakisaka nafasi ya kufuta gundu ya miaka 52 ya kusubiri (walitwaa kombe hili mwaka 1966). Croatia wao ndio kwanza wameianza hii safari.