Kombe la Kagame lachelewesha dili la Chilunda Hispania

Muktasari:

  • Chilunda amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo ambayo mchezaji mwingine wa  Azam FC,  Farid Musa anaichezea.

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Idd ‘Chilunda’ ataondoka nchini kwenda kujiunga na timu yake mpya ya Tenerife FC mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kumalizika Julai 13.

Chilunda amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo ambayo mchezaji mwingine wa  Azam FC,  Farid Musa anaichezea.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa mchezaji huyo, Phillip Arando, alisema kila kitu kimewekwa sawa kati ya Azam FC na Tenerife FC, hivyo mchezaji huyo ataondoka hivi karibuni baada ya michuano ya Kombe la Kagame kumalizika.

''Shaaban tayari ana mkataba wake na Tenerife na taratibu zote amekamilisha, kilichobaki ni kumaliza kuitumikia klabu yetu kwenye michuano ya Kagame kisha asafiri kwenda Hispania kwaajili ya kuanza maisha mapya ya soka la kimataifa'', alisema Arando.

Arando aliongeza kuwa wao kama timu wataendelea kutengeneza vipaji hata kama timu hazitawanunua moja kwa moja lakini kwa vipaji vya nyota hao wataendelea kuwaruhusu wakacheze kwa mkopo.