Tegete abeba zigo Majimaji

MAJIMAJI ndio imerejea zake mchangani na msimu ujao itakuwa na kibarua cha kusaka nafasi ya kurudi Ligi Kuu Bara, lakini mabosi wake wameumizwa kichwa wakatoka na matokeo hayo.

Kwa kauli moja mabosi hao wameamua kuwabakiza kikosini wachezaji 14 akiwemo straika matata wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete ili kuhakikisha inarudi Ligi Kuu Bara fasta tu badala ya kuanza kusajili wapya.

Wachezaji hao walikuwa na kikosi hicho kilichoshiriki ligi kuu msimu uliopita, ambapo Simba ilibeba ubingwa huku Yanga wakipata tabu sana na kumaliza nafasi ya tatu.

Majimaji itaungana na Njombe Mji ambayo ilishindwa kufurukuta kwenye msimu wake wa kwanza tu ligi kuu, baada ya kupanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza.

Meneja wa Wana Lizombe hao wenye maskani yao mjini Songea, Godfrey Mvula, amesema tayari mchakato wa usajili umekamilika na Tegete amekubali kusaini kandarasi ya mwaka mmoja.

“Wachezaji wengi mikataba yao ilimalizika msimu huu, lakini tayari asilimia 80 tuliokuwa nao wamekubali kusaini mikataba mipya ili kusaidia timu kuinuka tena,’’ alisema Mvula.

Alisema uwepo wa wachezaji hao kwa msimu ujao wa FDL unawapa imani ya kwamba, wataipigania Majimaji na kuirudisha VPL licha ya kuandamwa na historia mbaya ya kushuka na kupanda.

Hata hivyo, Mvula alidokeza kuwa kwa sasa wana mpango wa kuiendesha klabu hiyo kwa mfumo wa kampuni ili kuepukana na ukata na tayari kampuni ya Cowbell imeonyesha nia ya kushirikiana nao.