Kiungo Mudathir atua geto lile lile Azam FC

KIUNGO wa Azam FC, Mudathir Yahya aliyekuwa anakipiga kwa mkopo Singida United, amejikuta akirejea katika chumba kile kile ambacho alikuwa akikaa awali kabla ya kuondoka katika klabu hiyo.

Mudathir ameliambia Mwanaspoti baada ya kusaini mkataba mpya sehemu ambayo kama ni nyumbani kwake amekuta amerudishwa chumba kile kile na kupangiwa Abdallah Kheri ambaye alikuwa anakaa naye tangu wote wajiunge na timu hiyo.

“Nashukuru Mungu baada ya kurejea nimerudi katika chumba kile kile nilichokuwa nakaa awali na Abdallah Kheri ‘Sebo’ ndiye tulikaa wote awali, lakini nilivyotua tu akanikaribisha katika chumba hicho,” alisema.

Akizungumzia mazingira hayo ambayo alikosekana kwa muda mrefu, alisema ni tofauti kwani aliondoka kijana mdogo na amerejea akiwa anajitambua zaidi.

Mudathir aliongeza kwamba haoni kama yupo sehemu ngeni kwani nyuso nyingi bado zimebaki zile zile.