Basata yamtega mwandaaji shoo ya Werrason

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza amesema hajapata malalamiko kutoka kwa mashabiki wa burudani wanaotaka kutumia tiketi zao walizokata mwezi Aprili kwa ajili ya onyesho la Werrason linalotarajiwa kufanyika tena hapa nchini.

Mngereza alidokeza kwamba taarifa aliyokuwa nayo hapo awali kwamba mashabiki waliokata tiketi zao, wazitunze na ndizo zitatumika onyesho litakapofanyika.

Pia alisisitiza kwamba iwapo atapata malalamiko ya watu waliokata tiketi hapo watachukua hatua zaidi kwa mwandaaji ili kufuatilia tamko lake kuwa watu watunze tiketi zao na watazitumia onyesho litakapofanyika.

Alisisitiza kuwa Basata haiwezi kuamua jambo bila kupata malalamiko ya tiketi huku akishauri kwamba kauli ya waandaaji kuwa tiketi zitenzwe ndiyo  ilipaswa kuzingatiwa.

Ishu yenyewe ipo hivi. Unakumbuka ile shoo ya Werrason iliyoahirishwa mara tano na kushindwa kufanyika kutokana na mvua za masika zilizopiga jijini Dar es Salaam kwa takribani siku nne mfululizo, mkali huyo wa masauti anatua tena kutikisa jukwaa la Life Park Mwenge kwa mara nyingine tena, lakini mashabiki wanatakiwa kukata tiketi mpya ili kumuona.

Wakati kukiwa na ujio wa mwanamuzikio huyo, mwandaaji wa shoo hiyo, Yale Ngos amesema hazitambui tiketi za mashabiki zilizokatwa wakati huo ambapo shoo haikufanyika hivyo wanaotaka kumuona wanapaswa kukata tena.

Hata hivyo, mwandaaji huyo hapo awali wakati wa tamasha ambalo halikuweza kufanyika, aliwaahidi wapenzi ana mahabiki hao kuwa wote waliokata tiketi waendelee kuzitunza kwani, ndizo zitakazotumika tamasha hilo litapofanyika kipindi hicho lakini hadi dakika ya mwisho tamasha halikufanyika.

Ilikuwa kama sinema ya aina yake, awali shoo hiyo ilikuwa ipigwe kwenye ukumbi wa Escape one, ni kama kitumbua kiliingia mchanga kutokana na wajanja wa mjini kuchonga tiketi kibao za dili hata hivyo waandaaji walishtukia mapema mchezo mzima.

Wakati waandaaji hao wakipambana kujua jinsi gani ya kutatua tatizo hilo, siku yenyewe ya shoo mambo yakaharibika tena katika ukumbi wa  Escape one baada ya mvua mkubwa kunyesha. Pia hata walipobadilisha ukumbi hali ilikuwa hivyo hivyo mambo yaliharibika.

Mapema mwezi Aprili mwaka huu, waandaaji wa shoo ya mwanamuziki huyo walitangaza ujio wake na mashabiki wa mwanamuziki huyo walikuwa wakimsubiri kwa hamu.

Licha ya Werrason kutua jijini Dar es Salaam,  kutokana na mvua zilizokuwa zinanyesha mfululizo, shoo hiyo haikufanyika baada ya kuahirishwa kwa takriban mara tano.