Lukaku, Hazard waongoza mauaji Russia

KWANI kuna habari gani! Straika Romelu Lukaku na winga anayeteleza kama kambale Eden Hazard kila mmoja alipiga mbili kabla ya Michy Batshuayi kuja kupiga la mwisho wakati Ubelgiji walipoichapa Tunisia 5-2 katika mchezo wa fainali za Kombe la Dunia wa Kundi G uliofanyika jana Jumamosi huko Moscow, Russia.

Hadi dakika 51, tayari wawili hao Lukaku na Hazard kila mmoja ameshatupia mbili wavuni, huku Tunisia ilipata mabao yao ya kujifariji kupitia kwa Dylan Bronn na Wahbi Khazri na kukusanya virago kwa sababu wameshachapwa mechi mbili na wenzao Ubelgiji wakitinga kwenye hatua ya 16 bora.

Kwa matokeo hayo, yanafanya mechi hiyo kuwa ndiyo iliyoshuhudiwa mabao mengi zaidi tangu kuanza kwa fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia baada ya mabao saba kutinga wavuni. Mechi nyingine iliyokuwa na mabao mengi ni ile ya Hispania na Ureno iliyomalizika kwa sare ya 3-3, wakati Russia wenyewe walihusika kwenye mechi yenye mabao mengi pia wakati walipoichapa Saudi Arabia 5-0 kwenye mechi ya kwanza kabisa ya ufunguzi wa fainali hizo.

Mambo yangekuwa mabaya zaidi kwa Tunisia kama si Batshuayi kugongesha mwamba kabla ya kufunga bao lake ambalo lilikuwa la mwisho kwa upande wa Ubelgiji kwenye mehci hiyo. Ilikuwa siku nzuri kwa mashabiki waliojitokeza kwenye mechi hiyo kila wakati kunyanyuka kwenye viti vyao kushangilia mabao wakifanya hivyo mara saba.

Mechi nyingine ya kundi hilo itafanyika leo Jumapili kwa England kukipiga na Panama, huku England wakisaka ushindi ambao utawapeleka kwenye nafasi ya 16 bora baada ya kushinda mechi yao ya kwanza mbele ya Tunisia.

Katika michezo mingine iliyopigwa jana, Toni Kroos alifunga bao la jioni kuwafanya mabingwa watetezi Ujerumani kupata ushindi wao wa kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kuwachapa Sweden 2-1. Sweden ndio waliokuwa wa kwanza kufunga bao kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Ola Toivonen, lakini Marco Reus akaja kuisawazishia Ujerumani mapema kipindi cha pili kabla ya Kroos kufunga chuma cha pili kwenye dakika za majeruhi. Ushindi huo unafufua matumaini mapya kwa Ujerumani katika kutinga hatua ya 16 hivyo watahitaji kushinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Korea Kusini, ambao tayari wameshatupwa nje ya michuano. Sweden wao watacheza na Mexico, ambao tayari wameshatinga kwenye hatua ya mtoano, baada ya kushinda mechi yao dhidi Korea mabao 2-1.