#WC2018: Mitindo ya nywele iliyobamba Russia 2018

KOMBE la Dunia la huko Russia la ukweli mwanangu, hadi sasa kumeshashuhudiwa mabao makali si mchezo.

Cheki kama lile bao la Dries Mertens alilofunga dhidi ya Panama, Cristiano Ronaldo dhidi ya Hispania, Luka Modric dhidi ya Argentina au Ahmed Musa dhidi ya Iceland.

Hayo ni kuyataja kwa uchache tu mabao makali yaliyofungwa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia ambapo fainali zake sasa zimezidi kugonga na upinzani kuwa mkali. Hakuna kibonde, timu zinapata ushindi kwa mbinde!

Wakati hilo likiendelea kuna mambo mengine matamu yanayowafanya mashabiki kupata burudani ya ziada kupitia kwa staili za nywele za wanasoka waliopo kwenye fainali hizo. Kuna baadhi wamependeza na staili zao za nywele, lakini wengine wameonekana kama vituko tu. Hii ni kawaida kila inapofika michuano mikubwa kama hiyo ya Kombe la Dunia, lazima kunakuwa na staili za nywele kutoka kwa wachezaji zinazoacha gumzo, kama ile staili ya Ronaldo de Lima wa Brazil kwenye fainali za 2002 zilizofanyika Japan na Korea Kusini. Hivi hapa staili za nywele zilizoonekana huko Russia kutoka kwa wachezaji hadi sasa.

Domagoj Vida (Croatia)

Staili ya nywele za beki huyo wa Croatia ni majanga. Vida, amenyoa pembeni na kuacha katikati nywele ndefu na kuwa na mwenekano wa kipekee kabisa katika kikosi chake na hakujali kama staili hiyo imempendeza au la. Vida amenyoa pembeni, kisha katikati kuna nywele kubwa na kisogoni ameweka mkia mrefu wa nywele. Ni staili ya peke yake.

Neymar (Brazil)

Staili ya nywele aliyoibuka nayo Neymar katika fainali hizo za Russia imekuwa gumzo. Kuna wanaomkejeli ni kwamba amezifanya nywele zake zionekana kama tambi vile kwenye sahani. Neymar amezifanya nywele zake kuwa ndefu sehemu ya mbele, kisha amezipiga rangi na kuziweka nyingi kama vile ni tambi. Kwenye Kombe la Dunia 2014 aliibuka na staili kama ile ya Mohawk, lakini safari hii amekuja kuvingine kabisa.

Keisuke Honda (Japan)

Staa wa Japan, Keisuke Honda ameibuka na staili yake matata katika fainali hizo za Russia. Staili ya Honda inataka kufanana kama na ile ya kipindi kile cha Bobby Charlton. Lakini, alichokifanya Honda ni kwamba ameziweka nywele zake kuwa kubwa, kisha akazinyoa upande mmoja wa sikio, kisha anazilaza ule upande mwingine na kisogoni pia kuwa na nywele kubwa pia. Staili yake inabamba pia.

Luka Modric (Croatia)

Kiungo wa Croatia, Luka Modric ni mmoja wa wachezaji wenye staili za kipekee kwenye fainali za Kombe la Dunia zinaendelea huko Russia. Staa huyo wa Real Madrid amezifanya nywele zake kuwa ndefu na kisha amekuwa akichana kwa kuzilaza pembeni kushoto na kulia na kisongoni na kisha ananweka kibanio kuzifanya ziwe kwenye mwonekano huo huo kwa muda wote wa mchezo. Ndiyo staili yake ya nywele aliyokwenda kutamba nayo huko Russia.

Anibal Godoy

(Panama)

Staa wa Panama, Anibal Godoy ameibuka na staili ya nywele kwenye fainali hizo za Russia akizifanya zionekane kama kichaka vile. Godoy amenyoa pembeni kushoto na kulia na kisogoni na kuacha katikati tu huko akizisimamisha nywele hizo kama kichaka kama sio blashi ya kusafishia viatu. Leo, Jumapili chama lake la Panama lilitarajia kumenyana na England katika mechi ya pili ya kundi lao kwenye fainali hizo za Russia.

Axel Witsel (Ubelgiji)

Kiungo wa Ubelgiji, Axel Witsel ameamua kupamba michuano ya fainali za Kombe la Dunia huko Russia kwa staili ya mtindo wa nywele wa kizamani sana, ameweka afro. Wachezaji wengine wenye afro kwenye fainali hizo za Dunia ni Marouane Fellaini, Willian na Marcelo, lakini mtino wa Witsel upo tofauti ni kama ule wa miaka ya sabini, ambapo watu walikuwa wakipiga suruali nyembambaa, shati linafunga vingiii kwenye ile mitoko ya zama hizo.

Mohamed Salah (Misri)

Staili yake ya nywele Mohamed Salah ilikuwa maarufu sana kwenye miaka ya 80. Mtindo huo ametamba nao kwenye kikosi cha Liverpool kabla ya sasa kwenda kutamba nao pia huko kwenye fainali za Kombe la Dunia. Nywele za Mo Salah ni nyingi hivi, halafu ni kama vile vimewekwa dawa na kukumbushia zama zile za akina Graeme Souness, Kevin Keegan, Phil Thompson na Phil Neal. Staili yake ni kama mwamamuziki wa funk.

Jerome Boateng

(Ujerumani)

Kwa umri wa Jerome Boateng miaka 29 bado kijana sana kuwa na mvi, lakini kwenye fainali hizo za Russia ameamua kuzichoma nywele zake kuonekana kama zina mvi. Amenyoa pembeni na kuacha katikati huku kwa namna alivyozichoma nywele hizo zinamfanya awe na mwonekano wa kizee ili tu kuwa tofauti kwenye fainali hizo za Russia zinazozidi kuwa tamu kila kukicha na namna michuano inavyozidi kwenda mbele.

William Troost-Ekong (Nigeria)

Staa wa Nigeria, Ekong ameamua kuja na staili ya nywele ambayo inamfanya ajitambulishe kwamba yeye ni raia wa nchi hiyo. Alichokifanya Ekong ni kupaka rangi ya kijani kwenye nywele zake kuwakilisha rangi za nchi hiyo kitu kinachomfanya kujiunganisha moja kwa moja na mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa hawaoni shida kupaka rangi mili yao kwa ajili ya kuisapoti timu yao ya taifa yenye pointi tatu hadi sasa baada ya kucheza mechi mbili katika fainali hizo za Russia.

Nordin Amrabat (Morocco)

Unakumbuka ile staili ya Michael Jordan? Kunyoa kipara, basi hiyo ndiyo staili aliyoibuka nayo beki wa kulia wa Morocco, Nordin Amrabat kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Amrabat ameondoa nywele zote kichwani, lakini akiacha ndefu kumfanya kuwa na mwonekno wa kipekee katika kwenye fainali hizo. Morocco mambo yao yamekuwa magumu kwenye fainali hizo.