Dogo anajichotea ujuzi wa Mwadini pale Azam

KIPA Benedict Haule aliyekuwa anaichezea klabu ya Mbao FC, amejikuta katika wakati mgumu tangu alipojiunga na kikosi cha Azam FC, hali ambayo imemfanya aanze kufikiria kuomba kutoka kwa mkopo.

Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya naye mazungumzo kwa kina kutaka kufahamu mengi kuhusu yeye tangu ameanza kucheza soka lake la ushindani nchini.

AZAM NDIO ILIYOMKUZA

Kipa huyo alisema alianzia kucheza soka katika kituo cha kukuzia vipaji, Kitayo SC kilichopo Kilimanjaro Moshi, baada ya hapo akajiunga na akademi ya Azam FC 2013-14 lakini baada ya kukosa nafasi aliamua kuondoka kwenda kutafuta nafasi kwingine.

“Nilikuwa timu B kipindi hicho lakini niliondoka baada ya kuona nafasi ya kucheza ni ndogo, nilienda kujiunga na Panone na niliipandisha Daraja la Kwanza kitu ambacho najivunia mpaka leo,” alisema.

Benedict aliongeza kwamba baada ya kutoka Panone alienda Costal Union lakini hakukaa sana kisha akaenda kufanya majaribio Mbao FC na kufuzu.

CHEKI ALIVYOCHOMOKA MBAO

Wengi walishangazwa wakati anaondoka katika kikosi cha Mbao, kwani walitarajia kumuona akiwa na kikosi hicho msimu huu, lakini ghafla wakaona mchezaji huyo amemalizana na Azam FC.

Kumbe Mbao wenyewe ndio walishindwa kumalizana na kipa huyo baada ya dau lao kuwa dogo kuliko ambalo alikuwa amewekewa mezani na Azam.

“Nilikaa mezani na uongozi wangu wa zamani (Mbao) ili kuona kama tunaweza kukubaliana kile ambacho nilikihitaji, hatukuweza kuafikiana na ndipo nikatua Azam ambayo naitumikia mpaka hivi sasa,” alisema.

CHANGAMOTO YA NAMBA YAMUUMIZA

Kila mchezaji anapenda kucheza ili kuzidi kukuza au kuendeleza kipaji chake alichonacho, basi hali hiyo imekuwa kikwazo kwa Benedict kwani amekuwa kipa chaguo la tatu mbele ya Razack Abarola na Mwadini Ally.

Haule alisema kwamba changamoto ya namba imekuwa kubwa hivyo amejikuta hafurahii maisha ndani ya klabu hiyo, hali iliyomfanya afikile kutoka hata kwa mkopo.

“Nitajaribu kuongea na mabosi wangu nione inakuaje lakini msimu ujao nitatafuta timu niende kwa mkopo ili nipate nafasi ya kucheza kwasababu nahitaji kucheza,” alisema.

AWAZA KUKIPIGA NJE

Upande wa makipa wanaocheza soka la Tanzania, ngumu kusikia wanacheza soka la kulipwa Ulaya na hilo halijajulikana shida kubwa ni nini lakini kwa upande wa Haule amefunguka kwamba mipango yake ni kucheza nje.

“Umri wangu ni mdogo sana mimi, bado nina ndoto nyingi hadi hivi sasa naamini kabisa nina uwezo wa kucheza nje na hii ni moja ya ndoto yangu kubwa na sio mimi tu bali mchezaji yeyote anatamani hilo,”.

Akizungumzia kuhusu upande wa makipa kushindwa kujaribu kutoka nje ya nchi, alisema hilo linatokana na makipa wengi kutothubutu wao binafsi.

“Muda mwingine sio mpaka mtu akufate akupeleke, unaweza wewe mwenyewe ukatafuta njia na kwenda kujaribu, ninaamini Mungu akinijaalia nitaonyesha mfano,”.

MWADINI, ABAROLA WAMPA MZUKA

Licha ya kwamba anasugua benchi ndani ya kikosi cha Azam baada ya kupata ushindani wa kutosha kwa Razack Abarola na Mwadini Ally, kipa huyo alifunguka kwamba wachezaji hao wamekuwa kama mwalimu kwake.

Aliongeza kuwa na wachezaji hao timu moja kumemfanya aongeze mbinu mbalimbali kwani hata kocha wao wa makipa amekuwa na mbinu tofauti ambazo anakuwa anawapa katika mazoezi yao ambayo wanakuwa wanafanya kila siku.

BENEDICT NI NANI

Benedict Haule ni mtoto wa Mzee Haule, aliyezaliwa Mkoani Songea 24-2-1995, katika familia yao ya watoto watano yeye peke yake ndio anacheza soka la ushindani kwani baba yake aliwahi kucheza soka ligi daraja la Tano, lakini hivi sasa kaka yake wa pili kuzaliwa anachezea timu ya Daraja la Pili, Kitayo SC.