Beki wa Liverpool awapa neno TFF, timu za Ligi Kuu

Beki wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia  akizungumza na Mhariri Mshiriki wa Mwananchi Angetile Hosea katika studio za MCL, alipotembelea kampuni ya Mwananchi Communication Limited jijini Dar es salaam Ijumaa June 22. Picha na Michael Matemanga

BEKI wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia ameshangaa kuona Tanzania ina kundi kubwa la vijana wenye vipaji vya soka lakini akashtuka aliposikia timu ya Taifa 'Taifa Stars' haifanyi vyema kwenye mashindano ya kimataifa.

Baada ya kubaini hilo, Hyypia akatoa darasa la mambo mawili ambayo yakifanyiwa kazi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini, huenda mambo yakaanza kuwa mazuri miaka michache ijayo.

Masuala hayo mawili yaliyotajwa na Hyypia ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku nne iliyoratibiwa na Benki ya Standard Chartered ni mchakato wa usajili wa wachezaji wa kigeni pamoja na uzalishaji wa makocha wa soka wenye kiwango cha juu.

Akizungumza katika ziara yake fupi aliyofanya katika makao makuu ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha gazeti hili sambamba na mengine ya Mwananchi na The Citizen, Hyypia akisema iwapo Tanzania itahakikisha kunakuwa na ufanisi kwenye maeneo hayo, soka lake litapiga hatua.