Mkataba mpya wa TFF, La Liga ulete tija kwa maendeleo ya soka

Rais wa TFF, Wallace Karia

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) juzi liliingia mkataba wa ushirikiano na Waendeshaji wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), makubaliano yanayoelezwa yatatumika kusaidia kuliendeleza soka letu ili lifikie kiwango cha juu kama ilivyo La Liga.

Makubaliano hayo yamekuja wakati Ligi Kuu Bara msimu ujao ikitarajiwa kuanza ikiwa na klabu 20 kutoka 16 zilizokuwa kwa misimu kadhaa sasa, jambo ambalo kama kweli litatumiwa vyema na TFF na washirika wao ni wazi soka letu litasonga mbele.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo hususan soka, linaupongeza uongozi wa TFF kwa kufanikisha dili hilo, likiaminia kitaleta tija kwa maendeleo ya soka letu ambalo kwa miaka mingi limedumaa licha ya wenyewe kujiona tupo juu.

Tunaamini yale yaliyopo kwenye mkataba huo yatafanyiwa kazi kwa ufanisi hasa ikizingatiwa, makubaliano hayo yanahusisha soka kwa jumla bila kujali kama ni Ligi Kuu, soka la wanawake, vijana ama michuano mingine ilimradi ni soka la Tanzania.

Kitu cha muhimu kwa viongozi wa TFF ni kusimamia na kuhakikisha makubaliano hayo yanaleta tija kwa manufaa ya soka la Tanzania na hasa kuifanya Ligi Kuu ijitegemee kama alivyonukuliwa Msemaji wa TFF, Clifford Mario Ndimbo.

Hakuna siri, soka letu lipo chini na limekuwa likiendeshwa kwa mazoea wakati nchi nyingine zimekuwa zikiendesha soka lao kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia na ndiyo maana wametuacha mbali.

Ikikumbukwe Tanzania haijawahi kushiriki michuano yoyote mikubwa tangu Taifa Stars iliposhiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 na ile ya Wachezaji wa Ndani (Chan) 2009, huku klabu zetu zikiishia kuwa wasindikizaji kwa wenzao.

Mafanikio machache tuliyopata ya kufika fainali za CAF kwa Simba katika michuano ya Kombe la CAF 1993 na kushindwa kwa miaka karibu 40 kutua katika fainali za Afcon tu, achilia mbali kucheza fainali za Kombe la Dunia iwe chachu ya kusimamia mkataba huo na mabosi wa La Liga kuliinua soka letu.

Tungependa kuona mara baada ya kumalizika kwa makubaliano hayo baina ya TFF na watu wa La Liga, klabu zetu nazo ziwe tishio katika soka la Afrika kwa kuondoka katika kushangilia kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika badala yake tuanze kutembea kifua mbele kwa timu zetu kufika fainali na kubeba mataji.

Tunaamini ndani ya makubaliano hayo ya kutaka kuisimamisha ligi yetu iwe bora na imara ni dhahiri, ubabaishaji na mambo mengine yaliyochangia kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa ya ovyo yanarekebishwa.

Kwa mfano panga pangua ya kila mara ya ratiba ya ligi hiyo na maamuzi ya kushtukiza ya Kamati za TFF zinapaswa kuepukwa ili kusaidia kuwafanya mabosi wenzao wa La Liga kuongeza mkataba mwingine mpya siku za mbeleni.

Kwa mkataba huu mpya ulioingiwa TFF tunaamini mambo hayo yaliyokuwa yakiitibua ligi yetu na soka la Tanzania kwa jumla yanapungua kama sio kuondoka kabisa na kulifanya soka letu litoke mahali lilipo na kusonga mbele kushindana na nchi nyingine.

Hata hivyo, mkataba huo wa TFF uchochee pia klabu zetu kuanzisha ushirikiano na klabu za La Liga ili kusaidia kuwapa mbinu za kutoka mahali zilipo na kwenda na wakati ikiwamo kujifunza namna klabu za Hispania zilivyofanikiwa kutawala soka la Ulaya na Dunia kwa jumla.

Msisitizo wetu, mkataba huo ulete tija na mafanikio kwa soka la Tanzania sambamba na klabu zetu na wachezaji kwa jumla.

Nyota wa Tanzania wamekuwa wakisuasua kutoka nje ya nchi wakati mwingine kutokana na soka letu kutovutia klabu za nje, lakini kama kila kitu kitakaa sawa ni wazi tutashuhudia akina Mbwana Samatta na Farid Mussa wengine wakitapakaa Ulaya.

Aidha klabu zetu zinaweza kujifunza namna ya kujiendesha kisasa kama klabu zilizopo La Liga na katika ligi nyingine na mwishowe kulifanya soka letu lipae juu.

Hii ni nafasi muhimu kwa soka letu kupaa na kuleta mabadiliko mapya yatakayosaidia kuifanya Tanzania sio kujitangaza tu duniani, lakini pia litasaidia kufungua milango kwa nyota wetu kupata timu nje ya nchi.

Ndio maana tunasisitiza mkataba huo wa TFF na La Liga ulete changamoto zitakazoliinua soka letu kimataifa na kuwaneemesha nyota wetu.