Majimaji, Ndanda ni vita ya kubaki Ligi Kuu leo

Mwanza.Wakati Ligi Kuu Bara ikitarajia kufika tamati leo Jumatatu, vita kali itakuwa katika viwanja vya Songea na Nangwanda Sijaona kati ya Ndanda na Majimaji kupambana kukwepa janga la kushuka daraja.
Tayari Simba imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo, ambapo kwa sasa Azam na Yanga wao wanapambania nafasi ya pili,huku Njombe wakiwa tayari wameshashuka daraja.
Vita kati ya Ndanda na Majimaji inavuta hisia za wadau wa soka kuelekeza macho na masikiko yao kujua nani atabaki Ligi Kuu msimu ujao au wa kumfuata Njombe Mji Daraja la Kwanza.
Hadi sasa Ndanda wapo nafasi ya 14 kwa pointi 26, huku Majimaji wakiwa na alama 24 katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Ndanda ambao wametoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui watakuwa wenyeji dhidi ya Stand United, huku Majimaji wakiwa na kazi ngumu kuwakabili Mabingwa wapya Simba.
Kocha wa Ndanda, Mlale Hamsini alisema kuwa akili na mawazo yao ni kwenye mchezo huo muhimu kuhakikisha hawafanyi kosa kwani wakijichanganya tu basi inakula kwao.
“Nimekaa na wachezaji wangu nimewapa maelekezo nimeona wamenielewa, kwa hiyo nguvu, akili na mawazo yote ni kupata ushindi dhidi ya Stand United kesho (leo),” alisema Hamsini.
Naye Straika wa Majimaji, Marcel Boniventure alisema kuwa licha ya kuwa na kibarua kigumu cha kumkabili Simba, lakini wamejiandaa kisaikolojia kuhakikisha wanashinda.
“Mchezo hautakuwa rahisi, Simba wameonekana msimu huu kuwa wagumu, lakini tumejiandaa vizuri na nia yetu ni kushinda ili kukwepa rungu la kushuka Daraja,” alisema Boniventure.