Iniesta aanza kwa kishindo Japan

Muktasari:

Iniesta alijitokeza mbele ya mashabiki muda mfupi uliopita akiwa amevalia jezi namba 8 kama aliyokuwa akiitumia akiwa na Barcelona.

Maisha mapya na mashabiki wapya unaambiwa. Kiungo fundi wa soka aliyedumu ndani ya wababe wa Catalunya kwa miaka zaidi ya 20, Andres Iniesta ametambulishwa kwa mara ya kwanza kwa mashabiki akiwa ndano ya uzi wa Vissel Kobe kule Japan.

Umati wa mashabiki zaidi ya 4000 ulikuwa ndani ya uwanja wa klabu hiyo wa Noevir, kwa ajili ya kumshuhudia kiungo huyo ambaye ameondoka kwenye soka ushindani barani Ulaya huku akiwa kwenye orodha ya viungo watano bora kwa sasa.

Iniesta alijitokeza mbele ya mashabiki muda mfupi uliopita akiwa amevalia jezi namba 8 kama aliyokuwa akiitumia akiwa na Barcelona.

Kama kawaida, alianza kwa kusalimia mashabiki kisha akakamata gozi la ng’ombe na kuanza kuonyesha mautundu yake kwa dakika kadhaa kisha akawapa zawadi ya mpira huo huku akipunga mkono kuonyesha heshima kwao.

Akizungumza na mashabiki hao, Iniesta alisema kuwa ni amejiunga na klabu hiyo kutokana na kuvutiwa na kwamba, atahakikisha anafanya kila linalowezekana kuipa mafanikio.

Amesema anafahamu ana kazi kubwa mbele, lakini anafahamu jukumu la kuifanya Vissel kuwa moto na kushinda taji la bara la Asia.