Beckham: Wapigeni tu hao Liverpool

Muktasari:

Beckham, ambaye ameichezea Man United miaka kibao tena kwa mafanikio akishinda mataji yote makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutimkia Real Madrid mwaka 2003, ameonyesha bado anaichukia Liverpool kama ulivyo ushindani wa klabu hizo mbili zenye mafanikio katika soka la Kiingereza.

Si unajua kwamba, David Beckham, Garry Neville na mastaa kibao wa Manchester United hawaipendi Liverpool? Sasa Beckham ameshindwa kujizuia na kuweka uzalendo pembeni akiwapa mzuka Real Madrid kuwachapa Liverpool mabao ya kutosha na kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baadaye leo usiku.

Beckham, ambaye ameichezea Man United miaka kibao tena kwa mafanikio akishinda mataji yote makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutimkia Real Madrid mwaka 2003, ameonyesha bado anaichukia Liverpool kama ulivyo ushindani wa klabu hizo mbili zenye mafanikio katika soka la Kiingereza.

Tayari Real Madrid na Liverpool zipo mjini Kiev kusubiri kuona nani ataibuka mbabe, lakini Beckham amemtaka swahiba wake, Zinedine Zidane kupanga kikosi cha kazi ili kuhakikisha anabeba taji hilo.

“Nataka kumtaki kila la kheri Zizou a.k.a the boss na wachezaji wote kwenye mchezo wa leo, lakini tafadhalini sana naomba muwapige hao Liverpool,” amesema Becks.

Real Madrid inaingia uwanjani kusaka taji la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya na taji la 13 tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mikubwa barani Ulaya. Liverpool kwa upande wake inasaka taji la tano kwenye historia yake ya mashindano hayo.

Msimu huu Liverpool wamekuwa moto kwelikweli, wamemaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England.