Sportpesa yamwaga pesa Simba

Dar es Salaam: Mfuko wa Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba umezidi kunona baada ya wadhamini wao wakuu, SportPesa  kuwakabidhi kiasi cha Sh 100 milion katika hafla fupi ya kukabidhi ubingwa huo wa msimu wa 2017/18 kwenye makao makuu ya ofisi zao Masaki jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas  amewapongeza Simba kwa kutwaa ubingwa huo ambao ni mara ya 19.

"Simba imeitendea haki nembo yetu ya SportPesa, tunaamini kuwa udhamini wetu umekuwa chachu ya kutwaa ubingwa huo. Tunachokifanya leo ni kutimiza moja ya ahadi zetu tuliyotoa wakati tunasaini mkataba mwezi Mei mwaka jana kuwa tuna bonasi ya shillingi Milioni 100 endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa, "amesema Tarimba.

Akiongea kwa niaba ya Simba, Kaimu Rais, Salim Abdallah 'Try Again' ameshukuru SportPesa kwa kuwa nao bega kwa bega toka wawe miongoni mwa  wadhamini wa klabu hiyo kongwe nchini.

"Tulifanya maandalizi mazuri msimu huu kuanzia kwenye ngazi ya uongozi hadi benchi la ufundi na ndio maana sio jambo la ajabu kuwa mabingwa," amesema Abdallah.

Simba ni miongoni mwa timu nane zitakazo shiriki mashindano ya SportPesa nchini Kenya kuanzia Juni 3-10, nyingine ni Yanga, Singida United, JKU za Tanzania, Gor Mahia, AFC Leopards, Kakamega Home Boys na Kariabangi Shark za Kenya.