Mtanzania ajipanga kunyakua taji mpira wa meza Kenya

Dar es Salaam.  Mchezaji chipukizi wa mchezo wa mpira wa meza nchini, Sara Alidina anaanza kampeni ya kutwaa ubingwa wa  vijana wa mchezo huo nchini Kenya yaliyopangwa kuanza leo mjini Mombasa.

Sara (14) anawania taji hilo akiwakilisha jiji la Mombasa. Sara ambaye anasoma Shule ya Aga Khan Academy ya mjini Mombasa, anashiriki katika mashindano hayo kwa mara ya pili ambapo mwaka jana alifanikiwa kuingia fainali, lakini akashindwa kucheza kutokana na kuugua ghafla.

Kutokana na kufanya vizuri mwaka jana, waandaaji wa mashindano hayo wameamua kumshindanisha Sara kwa wacheza mpira wa meza wenye miaka chini ya 18, jambo ambalo limemhamasisha mchezaji huyo kufanya vyema.

Akizungumza  jijini jana, baba wa mchezaji huyo, Rahim Alidina alisema kuwa Sara amejiandaa vizuri katika mashindano hayo na anaamini atafanya vyema katika mashindano  hayo.

Alidina alisema kuwa Sara amejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo na wanarajia kufanya vyema. Alisema kuwa mwaka jana alifadhaika sana kutokana na kuugua huku akiwa na nafasi kubwa ya kufanya vyema katika mashindano hayo.

“Nimatarajio yetu kuwa atafanya vyema pamoja na kuwekwa katika kundi la watu ambao wamemzidi umri, hii imemjenga sana kutokana na ukweli kuwa  ndoto yake ni kufanya vyema katika mashindano,” alisema Alidina.

Alisema kuwa lengo ni kushinda na kuitangaza nchi, shule yake na Jimbo la Mombasa ambalo kwa sasa anaishi na kutokana na kusoma huko.

Alifafanua kuwa mashindano hayo ni magumu sana kutokana na ukweli kuwa wachezaji wengi wa mchezo huo wa Kenya wanashiriki.