Karia amshukuru Rais Magufuli

Dar es Salaam: Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania  TFF,  Wallace Karia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  John Magufuli kukubali kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kupokea makombe mawili la mshindi wa pili Kombe la Dunia la Watoto wa Mtaani na Ubingwa wa Cecafa kwa vijana chini ya miaka 17.

Karia amesema, wa niaba ya TFF  anapenda kumshukuru, Magufuli kukubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.

"Tumefarijika kwa Rais Magufuli kuungana na Wanamichezo na kuzungumza nao. Alichozungumza tumekipokea na tunaahidi tutakifanyia kazi kwa vitendo katika kuunga mkono jitihada zake za dhati kuona mpira wa miguu unapiga hatua,"amesema.

Amesema, tunaamini Wanamichezo wengine nao wataunga mkono jitihada hizo za TFF ili kufanikisha lengo.

"TFF tutahakikisha tunasimamia mpira wa Tanzania kwa kuongozwa na sheria, kanuni na utaratibu na hatutakubali kuona mtu anakwenda kinyume na kutaka kuvuruga taswira nzuri ya Mpira tuliyoanza kuijenga katika kipindi kifupi tulichoingia madarakani,"amesema.

Ameongeza kuwa wanaamini ushirikiano wa TFF na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli utafikia malengo kwa pamoja.

"Serikali ya awamu ya tano imekuwa na ushirikiano mkubwa na TFF katika kufanikisha masuala mbalimbali ushirikiano ambao hakika utaleta matunda zaidi.  Tunaamini kuwa timu zetu za Taifa zitafanya vizuri kama ambavyo timu yetu ya Vijana U17 Serengeti Boys ilivyofanya vizuri na kuchukua Kombe nchini Burundi na ya Wasichana ya kituo cha TSC kwenye fainali  za kombe la dunia la Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu,"amefafanua.

"Hakika ni mfano wa kuigwa mpaka kwenye ngazi ya klabu kwa kushinda mataji mbalimbali na mwisho namuhakikishia Rais  tutaendelea kusimamia mpira wetu ipasavyo kwa kushirikiana na Serikali  kwenye kila eneo linalohitaji msaada wa Serikali."