DSTV kurusha matangazo Kombe la Dunia kwa Kiswahili

Muktasari:

Kombe la Dunia ni mashindano makubwa zaidi duniani ambayo huwa yanafanyika kila baada ya miaka minne, mara ya kwanza kufanyika kwa kombe hilo ilikuwa Julai 30, 1930 nchini Uruguay.

Dar es Salaam. Zikiwa zinaendelea kuhesabika siku kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, Kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia king’amuzi cha DSTV  wanatarajia kurusha matangazo ya mashindano hayo moja kwa moja kutoka Russia kwa lugha ya Kiswahili.

Akizungumza juzi, Serena Hoteli jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa kurusha matangazo hayo, Maneja matukio wa Multichoice Tanzania, Ronald Shelukindo alisema watakuwa na chaneli sita zitakazorusha mubashara mechi zote 64.

Kombe la Dunia ambalo litafanyila kwa mara ya kwanza, Ulaya ya Mashariki,  linatarajiwa kuanza rasmi kutimjua vumbi, Juni 14 kwa mchezo wa ufunguzi kati ya  wenyeji, Russia dhidi ya Saudi Arabia.

"Kila mchezo utakuwa Live kwa sababu tumetenga  chaneli hadi sita ambazo zitahusika na kombe hilo la Dunia kwa lugha mbalimbali ikiwemo lugha yetu ya Kiswahili, tutarusha matangazo yetu kwenye kiwango cha juu (HD).

“Watangazaji mahiri na wachambuzi wetu nchini watafanya kazi hiyo huku pia tukiwa na baadhi ya nyota wa Afrika kama vile Yaya Toure na Jay-Jay Okocha,” alisema Shelukindo.

Wanaotarajiwa kuhusika kwa utangazaji na uchambuzi kwa lugha ya Kiswahili ni Eddo Kumwembe, Oscar Oscar ‘Mzee wa Kaliua’ , Ibrahim Masoud ‘Maestro’, Ephraim Kibonde, Maulid Kitenge na Abubakari Liongo.

Miongoni mwa nyota wa zamani waliokuwa kwenye uzinduzi huo ni  Edibily Lunyamila, Mshambauliaji Mohammed Hussein 'Mmachinga', Ivo Mapunda, Abel Mziba, Sekilojo Chambua na Charles Mkwasa.