Cheki kikosi cha mastaa kilichotemwa Russia

KUNA mastaa ambao wapo fiti, lakini wametangazwa kuachwa katika timu zao za taifa huku mashabiki wakibaki midomo wazi. Mastaa hawa wanaweza kutengeneza timu yao na wakaenda kombe la dunia na kulichukua.

KIPA - Sergio Rico

Miaka miwili iliyopita kipa huyu wa Sevilla alikuwa katika kikosi cha Hispania ambacho kilishiriki katika michuano ya Euro 2016. Hata hivyo katika michuano hii ya kombe la dunia pale Russia atakuwa sebuleni kwake na familia akitazama mechi hizo.

Msimu mbovu wa Sevilla mwaka huu umeigharimu nafasi yake ambayo imekwenda kwa makipa, Kepa Arrizabalaga wa Athletic Bilbao na Pepe Reina wa Napoli.

Nelson Semedo

Katika msimu wake wa kwanza Semedo ametamba Nou Camp. Alicheza mechi 36 na kutwaa mataji mawili pale Barcelona. Hata hivyo, pamoja na kuonyesha kiwango kizuri huku mazoezini akicheza na staa kama Lionel Messi, kocha wa Ureno, Fernando Santos ameona haitoshi na nafasi yake imekwenda kwa beki wa Southampton, Cedric Soares.

Aymeric Laporte

Fikiria kuwa umenunuliwa kwa pauni 57 milioni tu halafu baada ya miezi mitano hauendi kombe la dunia huku ukiwa fiti. Kama vile haitoshi, chumvi ilitiwa kidonda zaidi kwa Laporte wakati mlinzi wa Arsenal, Laurent Koscielny alipoumia lakini bado kocha, Didier Deschamps hakuweza kumuita kikosini. Badala yake Deschamps aliamua kumuita staa wa PSG, Presnel Kimpembe.

Shkodran

Mustafi

Inawezekana hakuwa na msimu mzuri huku timu nzima ya Arsenal ikiwa ovyo, lakini staa huyu bado ni nguzo kubwa kwa Ujerumani kombe la dunia. Hata hivyo, upinzani ni mkubwa kwa walinzi wa kati ambapo kocha, Joachim Low amewaita Mats Hummels na Jerome Boateng.

Marcos Alonso

Imewashangaza mashabiki wengi wanaomfahamu staa huyu wa Chelsea ambaye ni hodari wa kuziona nyavu licha ya jukumu lake la ulinzi. Alonso alikuwepo katika kikosi bora cha msimu cha England, lakini kocha wa Hispania ameamua kumpuuza yeye na ameamua kusafiri na mlinzi wa kushoto wa Arsenal, Nacho Monreal. Inawezekana kuna kitu kikubwa amekiona lakini ni wazi kwamba Alonso atakuwa amechukia kwa kiasi kikubwa.

Adrien Rabiot

Mmoja kati ya viungo ambao uvutia mashabiki katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Kutokana na utajiri mkubwa wa eneo la kiungo Ufaransa si ajabu ndio maana kocha, Didier Deschamps alichukua maamuzi maguu ya kumuacha staa huyu wa PSG. Alicheza mechi 43 na kutwaa ubingwa wa Ufaransa msimu huu lakini bado Deschamps hakuona kama anastahili kupanda ndege kwenda Russia.

Radja Nainggolan

Mmoja kati ya viungo bora duniani kwa sasa. Imewashangaza wengi kuona kwamba kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez hakuliona hilo. Badala yake ameamua kwenda Russia na viungo wake akina Marouane Fellaini ambao kucheza kwao pale Old Trafford kulikuwa kwa shida.

Nainggolan amethibitisha kwamba maelewano yake na Martinez hayakuwa mazuri. Pamoja na yote haya bado ni ngumu kukubali kwanini Nainggolan ameachwa na Martinez.

Ruben Neves

Ndio alicheza katika Ligi daraja la kwanza, lakini hilo haliwezi kuwa kisingizio kwa kocha wa Ureno kumuacha Neves. Kiungo huyu ambaye alipelekwa Wolves kwa mpango maalumu na wakala wake, Jorge Mendes ambaye ni wakala maarufu wa soka wa Ureno, aliisaidia kwa kiasi kikubwa Wolves kupanda Ligi Kuu mapema. Alifunga mabao muhimu na kuonyesha soka la uhakika.

Anthony Martial

Mpaka alipopata majeraha au alipowasili staa wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez, Anthony Martial alionekana kuwa na msimu mzuri Manchester United.

Hata hivyo, katika raundi ya pili alionekana kudorora kwa kiasi kikubwa na uhusiano wake na Jose Mourinho ulionekana kufikia kikomo. Hii ilimpa nafasi Didier Deschamps kumtosa.

Mauro Icardi

Pengine ndiye mchezaji ambaye anaweza kukuacha mdomo wazi zaidi katika orodha hii. Nahodha huyu wa Inter Milan ndiye mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Italia akiwa na mabao 29 katika mechi 36.

Hata hivyo, Waargentina wameamua kwenda na Gonzalo Higuain ambaye alikuwa katika Ligi moja na Icardi lakini hakuweza kufikia mabao ya Icardi. Lakini, Argentina wanaweza kujivunia utajiri wa eneo la ushambuliaji ambalo lina Paulo Dybala, Lionel Messi na Sergio Aguero.

Alvaro Morata

Mwanzoni mwa msimu hakuna ambaye angeweza kuwaza kuwa Alvaro Morata asingekuwepo katika ndege ya Hispania ambayo itapaa kwenda Russia kwa ajili ya kombe la dunia.

Alianza vema Chelsea huku akifunga mabao muhimu lakini mbele ya safari fomu yake ilionekana kutoweka kabisa. Hii ilimpa nafasi kocha wa Hispania kumtosa mchana kweupe.

Katika benchi: Ralf Fahrmann, Alex Sandro, Hector Bellerin, Jack Wilshere, Mario Gotze, Karim Benzema na Alexandre Lacazette.