Ndio wazee wa kuteleza Simba

Muktasari:

  • Mpaka kufikia jana asubuhi Yanga walikuwa wameachwa nyuma kwa pointi 17 na Simba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku wakicheza michezo 29 na Wekundu wa Msimbazi wana michezo 30 wakisaliwa na mchezo mmoja.

KAZI imeisha na Simba ndio imeshakabidhiwa ndoo yao tena na Rais John Pombe Magufuli. Kilichobaki kule upande wa pili ni kukamilisha ratiba tu na kujaribu kuisaka nafasi ya pili, lakini wana kazi ngumu kwelikweli mbele ya Azam FC.

Mpaka kufikia jana asubuhi Yanga walikuwa wameachwa nyuma kwa pointi 17 na Simba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku wakicheza michezo 29 na Wekundu wa Msimbazi wana michezo 30 wakisaliwa na mchezo mmoja.

Simba msimu huu ilionyesha tangu mapema kwamba inautaka ubingwa hivyo ikafanya uwekezaji mkubwa unaofikia Sh 1.3 bilioni kusuka kikosi chake. Kila idara Simba ni moto na ndio sababu safu yake ya ushambuliaji imepachika mabao 61 na beki yake kuruhusu mabao 14 tu huku ikipoteza mechi moja jana dhidi Kagera. Simba ilifungwa bao 1-0.

Hata hivyo, Simba imebeba ubingwa huku baadhi ya wachezaji wakinyanyua kwapa kushangilia kombe hilo bila kutokwa jasho kabisa. Yaani hawa ni wachezaji wa kushiriki mazoezi tu.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa likiifuatilia Simba kwa karibu, linakuletea orodha yao.

EMMANUEL MSEJA

Kipa huyu aliyesajiliwa kutoka Mbao FC, usajili wake uliingia figisu tangu awali alipotambulishwa ni kipa kijana wakati akionekana umri umekwenda.

Alipotua Simba akatulizwa mbele Aishi Manula na amekosa nafasi hata ya kuwa kipa namba mbili.

Hata hivyo, katika Kombe la Mapinduzi Cup, alicheza mechi nne na kufungwa magoli manne.

JAMAL MWAMBELEKO

Alikuwa mtamu alipokuwa Mbao FC lakini tangu amejiunga na Simba, amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Asante Kwasi na Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, ambao wao wenyewe wamekuwa katika bato nzito ya kugombania namba.

Beki huyo, ambaye Mwanaspoti lilimpa jina la Rasta aliposajiliwa Simba, amekuwa akitumia muda mrefu benchi.

PAUL BUKABA

Ukimwangalia ni mchezaji mwenye umbo zuri, lakini hajapata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

Alisajiliwa akitokea OC Muungano inayoshiriki Ligi Kuu DR Congo, amekuwa katika wakati mgumu kwa Simba hii ambayo ilihitaji ubingwa kwa jasho na damu kwa muda mrefu.

Simba walikuwa wanahitaji ulinzi wa kutosha hasa baada ya kutumia mfumo wa 3-5-2, ulioweka walinzi watatu nyuma ambapo wachezaji wanatakiwa wacheze kwenye umakini katika ukabaji kama Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili na James Kotei mbavyo wamekuwa wakifanya .

Katika msimu huu ameanza katika mechi nne tu, lakini ameonyesha atakuwa na msaada mkubwa kutokana na ukomavu wake ambao ameuonyesha.

JUMA LIUZIO

Alitua Simba kwa mkopo katika kikosi cha Zesco United ya Zambia, lakini baadaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja.

Haukuwa msimu mzuri kwake kwani, alianza katika mechi mbili na kufunga goli moja dhidi ya Ruvu Shooting, ukiachana na zile ambazo alipata nafasi ya kuingia kama mchezaji wa akiba.

Hajawa chaguo la kwanza kwa kocha Pierre Lechantre kwani, hata hizo nafasi alizopata nafasi ya kuanza ilikuwa wakati wa kocha Joseph Omog aliyesepa zake.

ALLY SHOMARI

Alikuwa ni chaguo la kwanza katika kikosi cha Mtibwa Sugar, uwezo wake wa kupanda na kupiga krosi uliwashawishi mabosi wa Simba kuvunja benki na kumsajili.

Lakini, wakati huo huo akatua Shomari Kapombe kutoka Azam, baada ya usajili huo ndio kama walianza kumchimbia kaburi, Ally Shomari.

Shomari alikuwa hapati nafasi ya kuanza mara kwa mara licha ya kwamba, katika mzunguko wa kwanza alipata nafasi wakati huo Kapombe akiwa majeruhi ama anacheza nafasi ya Nicholas Gyan, ambaye alikuwa anacheza kama mshambuliaji na sasa beki wa kulia, ndio hutumika kucheza nafasi ya Shomari.

Uwezo wa Gyan katika kukaba na kupeleka mipira mbele ndio msumari kwa Ally.

MOHAMMED IBRAHIM ‘MO’

Mchezaji ambaye ana mnyambuliko wa hali ya juu. Anaweza kuuchezea mpira anavyotaka na kumfanya beki kuishiwa pozi kabisa.

Inasemekana utovu wa nidhamu na uvivu wa mazoezini ndio umechangia akose nafasi.

Mo hakuwa mtu wa kunyanyua kwapa huku akiwa ajakichezea kikosi hicho mechi nyingi za ligi kuu, lakini kutokana na kocha Lechantre kuhitaji wachezaji wapambanaji Mo amejikuta akisugua gaga.

MWINYI KAZIMOTO

Kiungo mkongwe ndani ya kikosi cha Simba, msimu huu naye anakuwa mchezaji anayechukua kombe bila kukichezea kikosi mechi nyingi.

Kazimoto, ambaye anamaliza mkataba wake msimu huu ndani ya kikosi hicho, kuna asilimia kubwa anaweza kutafuta timu nyingine huku akihusishwa kujiunga na klabu yake ya zamani JKT Ruvu.

MOHAMMED HUSSEIN

Usishangae lakini ndio ukweli wenyewe huu. Msimu uliopita alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi, lakini imekuwa tofauti na msimu huu.

Zimbwe Jr katika mzunguko wa kwanza alicheza ila haukuwa mzunguko uliokuwa na ushindani.

Mzunguko wa pili Simba walimsajili Asante Kwasi na kwenda kuchukua nafasi hiyo ya Zimbwe Jr, ambapo alijikuta akikalia benchi.

NIYONZIMA

Wakati anasajiliwa na Simba akitokea Yanga, wengi walishtushwa na usajili wake kwani hawakutegemea.

Lakini, tangu amesajiliwa msimu huu hajawa na msaada mkubwa kutokana na majeraha kumtibulia na kumfanya asikitumikie kikosi hicho.

Wastani wa mechi ambazo ameanza kwa kucheza hauzidi mechi 10 ukiachana na ambazo aliingia akitokea benchi.

WENGINE

Kipa Said Mohammed ‘Nduda’, licha ya kwamba alikuwa ni kipa namba mbili klabuni hapo bado alikuwa na wakati mgumu kwenye ligi kuu msimu huu.

Nduda ambaye alisajiliwa akitokea Mtibwa Sugar, tangu ametua katika kikosi cha Simba amekumbana na majeraha ambayo yamemfanya ashindwe kupeleka ushindani wa kutosha kwa Manula. Nduda alicheza jana na kufungwa bao na Kagera.

Kuna Salim Mbonde, ambaye licha ya kuwa ni beki imara lakini hakuwa katika wachezaji waliochangia ubingwa msimu huu kutokana na kushindwa kucheza mechi nyingi baada ya kusumbuliwa na majeraha.

Mavugo hajaingia asilimia zote humu, kutokana na mchezaji huyo kupigana katika mechi muhimu kama ya Lipuli na kufunga bao, mechi ambayo Simba walikuwa wanahitaji ushindi.