Bocco: Mbona Ulaya ni fresh tu

Muktasari:

  • Lakini, ndani ya msimu wake wa kwanza tu akiwa na Wekundu wa Msimbazi ameshaonyesha makali yake na kusaidia timu yake kumaliza ukame wa mataji ulioweka kambi klabuni hapo kwa miaka mitano mfululizo.

NAHODHA wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ wakati anaondoka Azam, wengi walimuona kama amefulia kwenye soka la Tanzania huku wengine wengine wakimuona anakwenda kumaliza soka lake.

Lakini, ndani ya msimu wake wa kwanza tu akiwa na Wekundu wa Msimbazi ameshaonyesha makali yake na kusaidia timu yake kumaliza ukame wa mataji ulioweka kambi klabuni hapo kwa miaka mitano mfululizo.

Bocco mpaka sasa amepachika mabao 14 huku akitengeneza pacha matata na hatari kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, akiwa sambamba na Emmanuel Okwi.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano naye ya kina ambapo, ameeleza mambo mengi na mikakati yake mipya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

KUJA KIVINGINE

“Ulikuwa msimu mzuri kwangu hasa ukizingatia nimetoka kufanya kazi sehemu moja kwenda nyingine. Nimetekeleza majukumu yangu kwa ufanisi na matokeo yameonekana. Ni kitu kikubwa sana katika maisha yangu ya soka,” anasema Bocco.

Bocco ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekutana na bahati kubwa kwani, katika msimu wake wa kwanza tu Simba, ameiwezesha kubeba ubingwa.

SOKA LA NJE

Ndoto kubwa ya wachezaji wa Tanzania kwa sasa ni kuvuka mipaka kwenda kucheza soka la kulipwa nje, lakini kwanza wamekuwa wakitafuta njia ya kuwafikisha huko. Harakati za wachezaji wa Kitanzania kusaka nafasi nje zimekuwa zikishika kasi na Bocco naye ana mipango yake unaambiwa.

Kama unadhani Bocco ameridhika kucheza soka lake Tanzania tu, basi utakuwa unajidanganya kwani huyu jamaa anawaza mbali kwelikweli. Bocco anaeleza kuwa, bado ana ndoto za kwenda kumaliza soka lake nje ya Tanzania na kwamba, hilo limekuwa likimpa mzuka kucheza kwa bidii na kuongeza kasi ya kupasia nyavuni.

“Nina uhakika nitamaliza soka langu nje ya Tanzania, Mungu ndio kila kitu kwangu na nina imani kuna siku mipango itakaa vizuri. Bado ninaweza kucheza soka la ushindani kwa miaka mingine zaidi ya mitano, sipoi kabisa,” anasema Bocco.

VIPI KUREJEA AZAM

Si unakumbuka Bocco alikuwa mmoja wa mastraika walioipandisha daraja Azam FC kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008, kisha akaibeba mabegani na kuipa mafanikio hadi kubeba ubingwa msimu 2013-2014 tena bila kupoteza mchezo hata mmoja, lakini baadaye aliondoka na kutua Simba.

Na kama kuna kitu ambacho Azam wanajuta kwa sasa na hali wanayopambana nayo basi ni kumuacha Bocco aondoke, lakini kama hufahamu basi ni kuwa straika huyu hafahamu kabisa kama anaweza kurudi tena Chamazi.

“Dah! Ni ngumu kuzungumzia hilo kwa sasa, siwezi kuongea kuhusu kuondoka kwangu Azam au kurejea,” alijibu kwa kifupi tu mshambuliaji huyo.

KUMBE NI SHABIKI WA OKWI

Inawezekana wengi walikuwa hawajui kabisa kuwa Bocco ni miongoni mwa mashabiki wa Okwi, ambaye msimu huu amekuwa mtamu kinoma. Okwi ameshatupia nyavuni mabao 20 na ndiye atakabidhiwa Kiatu cha Dhahabu.

“Okwi ni mchezaji wa kipekee sana pamoja na uwezo wake ni mkubwa, ni bahati kucheza naye kwa sababu ni mchezaji wa aina yake halafu nikimuona uwanjani tu huwa napata mzuka. Jamaa anaifanya kazi ya kusaka ushindi kuwa nyepesi sana uwanjani, ni sawa na Kipre Tcheche wakati tunacheza wote pale Azam,” anasema.

SIMBA YAMPA MAISHA

Kama ilivyo ndoto za wachezaji wengi wa Kitanzania kutamani kuchezea Simba, Yanga na Azam basi kwa taarifa yako hata kwa Bocco mambo yalikuwa hayo hayo. Jamaa alipata mzuka mwingi sana kuzichezea klabu kubwa na ndoto yake ilikuwa ni kukipiga Simba wakati huo akiwa Azam.

Bocco anafunguka kuwa, kujiunga kwake Simba kumebadili mambo mengi ikiwemo kupiga hatua kimaisha licha ya kuwa bado anacheza nchini.

“Kutoka sehemu moja hadi nyingine ni hatua katika maisha, kwangu hii ni hatua ingawa imekuwa hapa hapa Tanzania.”