Mourinho aonywa fainali ya FA,akipigwa na Conte itakula kwake

Muktasari:

  • FA linabakia taji pekee ambalo Kocha wa Chelsea, Antonio Conte anaweza kuondoka nalo msimu huu, na linabakia kuwa taji pekee ambalo Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anaweza kulitwaa msimu huu baada ya kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu, Kombe la Ligi na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

NI fainali. Keshokutwa. Ni Chelsea dhidi ya Manchester United pale Wembley kuwania ufalme wa FA msimu huu. Wote watakuwa wanasaka kuibuka na taji pekee la msimu huu baada ya kushindwa kutwaa chochote katika mataji mengine.

FA linabakia taji pekee ambalo Kocha wa Chelsea, Antonio Conte anaweza kuondoka nalo msimu huu, na linabakia kuwa taji pekee ambalo Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anaweza kulitwaa msimu huu baada ya kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu, Kombe la Ligi na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

United iliishia nafasi ya pili katika ligi wakati Chelsea imeondoka bila ya kutinga nafasi nne za juu na inatazamiwa kuachana na kocha wake, Antonio Conte hata kama ikifanikiwa kuchukua taji hilo la FA.

Lakini sasa staa wa zamani wa Arsenal, Charlie Nicholas amemuonya Mourinho kuwa anakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa mabosi wake kama atashindwa kulipeleka taji hilo Old Trafford jioni ya Jumamosi.

Nicholas, hata hivyo, amemuonya Mourinho ambaye ana historia ya kuwa ‘muuaji mzuri wa mechi’ kwamba bodi ya timu hiyo inaweza kumgeuka na kuacha kumuamini kama atashindwa kuifunga Chelsea wikiendi.

“Hajakaribia hata kuwania tuzo ya kocha bora wa msimu, na kama hatatwaa Kombe la FA, basi atakuwa katika presha kubwa kutokana na historia yake ya kuwa muuaji mzuri katika mechi kama hizi,” alisema staa huyo wa zamani.

“Haonekani kuwa ametulia kama kocha wa United, na timu inaonekana kama dhaifu hii, amepata miezi 12 ya kuthibitisha ubora wake kwa sababu bado haijaiimarisha sana timu hii kwa jinsi inavyocheza,” alisema Nicholas.

Nicholas anaamini tofauti na ilivyokuwa zamani, siku hizi kocha huyo ameanza kupoteza hofu ambayo alikuwa anawajengea wapinzani wake kutokana na ushindi wake wa mara kwa mara kwa sababu amekuwa hapati matokeo mazuri mara kwa mara kama zamani.

“Naanza kudhani lile tishio la Mourinho kwa wapinzani linaanza kupotea. Na kama hatapata matokeo katika eneo hili la burudani, basi ni wazi atakuwa katika presha kubwa pale Old Trafford,” aliongeza staa huyo.

Wakati huohuo, staa wa Manchester United, Romelu Lukaku imethibitika kuwa atakuwa fiti kwa ajili ya pambano hilo na amerudi mazoezini juzi baada ya kwenda kwao Ubelgiji kupata tiba ya uhakika kuelekea katika pambano hilo.

Staa huyo aliumia kifundo cha mguu dhidi ya Arsenal Aprili 29, na angeweza kucheza hata katika pambano la Jumapili dhidi ya Watford lakini Kocha Mourinho alimpumzisha kwa ajili ya kujiandaa vizuri kwa pambano la Chelsea.

Lukaku, 25, amekuwa na msimu mzuri wa kwanza akiwa amehamia kutoka Everton kwa dau la Pauni 75 miloni akitokea Everton. Amefunga mabao 27 katika mechi 50 na amejitahidi kuziba pengo la staa wa msimu uliopita, Zlatan Ibrahimovic, ambaye ametimkia zake Marekani.

Pambano hilo linawakutanisha mastaa ambao waliwahi kufanya kazi zamani katika timu pinzani. Lukaku ni mmoja kati ya wachezaji ambao watakuwa wanakumbana na timu yao ya zamani sambamba na Nemanja Matic na Juan Mata ambao, waliwahi kukipiga Chelsea.

Kocha Jose Mourinho naye atakuwa anakumbana na timu yake hiyo ya zamani wakati kwa upande wa Chelsea, kiungo Danny Drinkwwater atakuwa anacheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani ambayo aliichezea akiwa mdogo.