USM Alger yaing'ang'ania Gor Mahia Kasarani

Nairobi. Jahazi la Gor Mahia ya Kenya katika mechi za kimataifa, limeendelea kuyumba baada ya kulazimishwa sare na USM Algiers ya Algeria, kwenye mchezo wa pili wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika, uliochezwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Kasarani Jijini Nairobi.

Hii ni sare ya pili kwa wawakilishi hao wa Kenya, kwani katika mchezo wa kwanza, walitoka sare ya 1-1 na Rayon Sports ya Rwanda, jijini Kigali. Mwenendo huu ni wa kutia hofu, kwani inawaweka katika wakati mgumu hasa ikizingatia mchezo unaofuata wanakutana na Yanga ya Tanzania.

Dalili za kuzama kwa jahazi la Kogalo zilianza kuonekana mapema, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika sehemu kubwa ya mchezo huo na kipindi cha pili, ikiwalazimu kucheza pungufu.

Katika dakika ya tano y mchezo, Gor Mahia walijikuta katika wakati mgumu shukrani kwa muamuzi aliyepotezea penalti ya wazi ya maadui baada ya Joash Onyango kumkwatua Mezianne Rehmanne ndani ya boksi.

Kogalo walifufuka baada ya tukio hilo na kufanya mashambulizi mfululizo katika lango la Algiers, huku kiungo mchezeshaji Francis Kahata na George Odhiambo Blackberry wakicheza gonga gonga za haraka na kuwachanganya viungo wa Algiers.

Katika dakika ya 14, mwamuzi aliwabania Gor Mahia penalti ya wazi baada ya mpira uliopigwa na Ephraim Guikan kumbabatiza beki wa USM Algiers, Abdelahoui Ayub, mkononi ndani ya eneo la hatari.

Katika dakika ya 22, jaribio la Gor Mahia, langoni mwa USM, halikuzaa matunda baada ya shuti la Guikan kupanguliwa na kipa wa USM, Mohammed Zemamouche.

Zikiwa zimesalia dakika chache kipindi cha kwanza kimalizike, Kahata aliunganisha krosi safi kutoka kwa George Odhiambo 'Blackberry' lakini mlinda lango wa USM alikuwa makini kuzuia jaribio hilo.

Katika dakika ya 73, Gor Mahia walinyimwa penalti nyingine baada ya George Odhiambo kuchezewa rafu na beki wa USM Algiers, Mohamed Benyahia. Dakika chache baadaye Ernest Wendo alifanya kazi kubwa kuzima jaribio la mashambulizi ya

kushtukiza kutoka kwa Abdelraouf Benguit.

Sare hiyo, inaiweka Gor Mahia kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D huku USM Algiers wao wakiendelea kukalia usukani. Rayon Sports ya Rwanda ipo katika nafasi ya tatu, huku Yanga ya Tanzania ikiburuza mkia.