Kenya kukipiga na Equatorial Guinea, Swaziland

Nairobi. Timu ya Taifa, Harambee Stars, inayonolewa na Mfaransa Sebastien Migne, itacheza mechi mbili za kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Mataifa Huru Afrika, dhidi ya Ghana, utakaopigwa mwezi Novemba Jijini Nairobi.

Huo ni mtihani wa kwanza kwa Migne tangu atue nchini kuchukua mikoba ya Paul Put.  Kenya itakipiga na Swaziland Mei 25, Uwanja wa Kasarani kabla ya kuwaalika Equitorial Guinea siku tatu baadaye.

Tangu atue nchini, kuchukua mikoba ya kuinoa Stars, Migne amekuwa na kazi kubwa ya kujenga kikosi imara akiwa na lengo la kufufua mchezo wa soka nchini.

Katika programu yake, mapema juma hili,  Mfaransa alianzisha kambi ya mazoezi kwa ajili ya kutambua vipaji vya soka nchini.

Mazoezi hayo, ambayo yalianza rasmi Mei 15 mwaka huu, katika uwanja wa Camp Toyoyo, ni kwa ajili ya kutengeneza kikosi kinachocheza soka la kisasa, muunganiko mzuri wa wachezaji wa ndani na maproo pamoja na kuhakikisha falsafa kucheza mpira wa burudani unawaingia wachezaji.

Wakati huo huo, Kenya imepanda nafasi mbili katika msimamo wa ubora duniani, kwa mujibu taarifa ya shirikisho la soka duniani, FIFA iliyotolewa mapema leo. Hata hivyo, hakujakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na kutokuwa na mechi zozote za kimataifa tangu mwezi Machi.