Lechantre ainasa Yanga SC

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanasposti, Lechantre alisema amekuwa akiifuatilia Yanga kupitia luninga katika mechi zake nyingi na kugundua kuna wachezaji watatu tu ndio tishio na wana nguvu kwenye kikosi hicho.

HUKU Simba wenyewe wanakwambia hawaachi kitu unaambiwa na kocha wake, Pierre Lechantre tayari ameanza mikakati kuhakikisha anabeba pointi zote tatu dhidi ya Yanga hapo Jumapili.

Yaani Mfaransa huyo kwa sasa yuko kwenye mikakati mizito kuhakikisha anaizamisha Yanga mchana kweupe na kuondoka uwanjani kifua mbele.

Akizungumza na Mwanasposti, Lechantre alisema amekuwa akiifuatilia Yanga kupitia luninga katika mechi zake nyingi na kugundua kuna wachezaji watatu tu ndio tishio na wana nguvu kwenye kikosi hicho.

Amemtaja Kelvin Yondan, Thaban Kamusoko na Obrey Chirwa kuwa ndio wamekuwa wakihusika mara nyingi kwenye ushindi wa Yanga na kwamba, kila mmoja ana uwezo wake.

Alisema Yondan ni mzuri kwa kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani na ana uwezo wa kuzima mashambulizi, wakati Kamusoko si mzuri katika kukaba, lakini ana uwezo wa kupiga pasi hatari.

“Chirwa ana matumizi mazuri ya nguvu, msumbufu na ana uwezo wa kufunga ndio maana alipata nafasi moja tu katika mechi tuliokutana nao mzunguko wa kwanza na kufunga bao la kusawazisha.

“Mbali na kuyaona hayo kupitia luninga, pia nilipata muda wa kuitazama Yanga mubashara dhidi ya Singida United, nilikuwa uwanjani na mengi ambayo siwezi kusema hadharani kwa sasa niliyaona.

Nimewapatia vijana wangu na ndio itakuwa silaha yetu uwanjani ya kuwachapa Yanga mapema tu.

“Yote haya nimeyafanya ili kuhakikisha tunapata ushindi ili kujiweka vizuri na ubingwa msimu huu, tunachukua ubingwa na hilo halina ubishi kabisa,” alisema Lechantre huku akionekana kujiamini kwelikweli ikiwa ni siku tatu kabla ya mpambano huo.