Mastraika 4 kumng’oa Ngoma Yanga

Muktasari:

  • Lakini, ili kuhakikisha wanafanya kweli kwenye michuano hiyo pamoja na Ligi Kuu Bara ambayo inaelekea ukingoni na maandalizi ya msimu ujao, tayari wameanza harakati za kuimarisha kikosi chao na sasa wanazungumza na mastraika wanne tofauti.

YANGA ndio wawakilishi pekee katika michuano ya Klabu Afrika na wameingia hatua ya makundi na sasa wanajipanga kuwakabili wapinzani wao, USM Alger (Algeria), Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sport (Rwanda).

Lakini, ili kuhakikisha wanafanya kweli kwenye michuano hiyo pamoja na Ligi Kuu Bara ambayo inaelekea ukingoni na maandalizi ya msimu ujao, tayari wameanza harakati za kuimarisha kikosi chao na sasa wanazungumza na mastraika wanne tofauti.

Washambuliaji hao ni Adam Salamba wa Lipuli, Arafat Djako wa Welaytta Dicha, Mnigeria Quadri Kola Aladeokun na Habib Kyombo wa Mbao na kama watanasa saini za mastaa hawa ni wazi Ngoma na Amiss Tambwe wataisoma namba. Yanga ili kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao wanaweza kumuacha Ngoma kutokana na rekodi zake za kuwa majeruhi, ambapo hajaonekana uwanjani tangu alipoumia goti tangu Septemba, mwaka jana.

Kwa upande wake, Tambwe anayesumbuliwa na goti naye anaweza kuingia katika orodha hiyo ya kupigwa panga kama mastraika hao watapatikana, lakini Yanga watalazimika kuwalipa fidia ya kuvunja mikataba yao kwani, inamalizika msimu ujao. Kanali mstaafu, Iddi Kipingu alisema kama Yanga watawapata washambuliaji hao wapya basi wanaweza kufanya mambo mawili, wakaingia moja kwa moja ama wakachemka.

“Yanga kweli haipo vizuri baada ya kukosekana kwa wachezaji wao majeruhi, lakini kama wanafanya usajili wa wachezaji hao wanatakiwa kuwapa hali ya kujiamini na si kama wanavyotaka wao kwa kutaka makubwa kutoka kwao kwa muda mfupi,” alisema.

“Kama watawaacha Ngoma na Tambwe ambao walifanya mambo mazuri basi wanatakiwa kuwalea vizuri wachezaji vijana wanaocheza kwa sasa ili kuwapa kitu tofauti,” alisema Kipingu. Nyota wa zamani wa Yanga Sekilojo Chambua alisema kama uongozi wa timu hiyo wakifanikiwa kuwanasa mastraika hao watakuwa wamepiga bao kwani, wataongeza nguvu hasa wakati huu wakishiriki michuano ya kimataifa.

Chambua alisema mwaka 1998, walishafanya hivyo kwa kuwaongeza Alphonce Modesti, Shaaban Ramadhani na Monja Liseka ambao waliongeza mzuka kikosini.

“Sina shaka na hawa mastraika wazawa, lakini wanatakiwa kujiridhisha na viwango vyao kwani kuwaacha Ngoma na Tambwe waliofanya vizuri na kuwachukua ambao, watashindwa kufanya hivyo watakuwa wamefeli,” alisema Chambua.