Kocha amtega Tshishimbi

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti Zahera alisema kabla ya kutua hapa alikuwa hamjui Tshishimbi, ambaye ni raia mwenzake wa DR Congo kauli ambayo pia ilitolewa na kiungo huyo, lakini kocha huyo akasema juzi wamekutana na akafanya naye kikao kifupi.

KOCHA Mwinyi Zahera tayari ameanza kazi jana jioni pale Bigwa mkoani Morogoro, lakini kabla ya kufika hapo amefanya kikao kimoja kifupi na kiungo wake Pappy Kabamba Tshishimbi akimpa jukumu zito ndani ya timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti Zahera alisema kabla ya kutua hapa alikuwa hamjui Tshishimbi, ambaye ni raia mwenzake wa DR Congo kauli ambayo pia ilitolewa na kiungo huyo, lakini kocha huyo akasema juzi wamekutana na akafanya naye kikao kifupi.

Zahera alisema katika mazungumzo yao alimwambia Tshishimbi kwamba, nafasi ya kulichezea taifa lake kwa mara ya kwanza ipo katika mikono yake, lakini kwanza anatakiwa kufanya kazi kubwa kuliko ile aliyowahi kuifanya wakati anajiunga na Yanga akitokea Mbabane Swallows.

Kocha huyo ambaye bado ni kocha msaidizi wa Congo, alisema Tshishimbi asitarajie kupendelewa kutokana na kwamba ni raia mwenzake badala yake kiungo huyo ndiye atakuwa na mateso katika utawala wake kwa kutakiwa kujituma na kuwa mfano kwa wengine.

“Sikuwa namjua Pappy (Tshishimbi) lakini kiongozi mmoja aliniambia kuna Mkongomani mwenzangu hapa na nikakutana naye tukazungumza kidogo kutambulishana,” alisema Zahera ambaye ujio wake ulifichuliwa na Mwanaspoti kama lilivyofanya kwa kocha aliyemtangulia George Lwandamina na wengine kufuata upepo.

“Nimemwambia sasa anatakiwa kufanya kazi hapa Yanga kama kweli anataka siku moja achezee kikosi cha taifa lake, hatakuwa anapendelewa hapa kwa kuwa mimi nipo hapa nimemwambia atateseka kwa kufanya kazi kubwa kuliko wengine na nidhamu ya hali ya juu.

Azuia mkataba afanye kazi

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wazito wa Yanga ni kwamba, Zahera alifanya kikao nao na kujadiliana nao mambo mbalimbali, lakini amesisitiza wala kusiwe na uharaka wa kumpa mkataba mpaka waukubali uwezo wake.

Bosi mmoja wa Yanga alisema kocha huyo ametua kambini Morogoro kuanza kazi mara moja na kwamba, yuko tayari atumie hata miezi mitatu akiwa na Yanga kuonyesha uwezo wake kisha ndiyo watarudi mezani kuzungumzia mkataba.

ATUA MOROGORO

Zahera alitua mjini Morogoro akiwa na baadhi ya vigogo wa Yanga akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika na kupelekwa Hoteli ya Kings Way na kupokewa na maofisa wengine.

Jioni Mcongo huyo alitua kwenye uwanja wa mazoezi uliopo Bingwa na kabla ya kuanza lolote aliteta kwa dakika kadhaa na Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Meneja wa timu, Hafidh Salehe kisha akaingia kazini jambo lililowafanya wachezaji kupandisha mzuka wakiamini kazi imeanza.