Bluefins yapeleka waogeleaji 26 Isamilo

Muktasari:

Mashindano hayo ya kila mwaka, yatashirikisha  timu nyingine tisa ambazo  zitachuana katika bwawa la ya Shule ya  Kimataifa ya Isamilo.

JUMLA ya waogeleaji 26 wa klabu ya Bluefins ya jijini Dar es Salaam watashiriki katika mashindano ya kuogelea ya Isamilo ambayo yamepangwa kuanza kesho Alhamisi mkoani Mwanza.

Mashindano hayo ya kila mwaka, yatashirikisha  timu nyingine tisa ambazo  zitachuana katika bwawa la ya Shule ya  Kimataifa ya Isamilo.

Mhasisi na Kocha Mkuu wa Bluefins,  Rahim Alidina amesema kati ya waogeleaji hao 10 ni wasichana na 16 ni wavulana na watachuana katika staili tano za mashindano hayo pamoja na relay. Staili hizo ni backstroke, butterfly, freestyle, Breaststroke, na Individual Medley (IM).

Alidina amewataja waogeleaji hao kwa upande wa wanawake ni pamoja na  Zianna Alidina, Muskaan Gaikwaad, Nihad Meghji, Aliyana Kachra, Aminaz Kachra,Sarah Shariff, Alexis Misabo, Niharika Mahapatra, Maryam Ipilinga na Lina Goyayi.

Waogeleaji wavulana ni  Isaac Mukani, Zac Okumu, Aaron Akwenda, Christian Fernandes, Burhanuddin Zavery, Moiz Kaderbhai, Parth Motichand na Vinaamra Dhoot.

Wengine katika orodha hiyo ni  Ayaan Shariff, Sahal Harunani, Hassan Harunani, Kaysaan Kachra, Revacatus Josephat, Jay Govindji, Delbert Ipilinga  na Mohameduwais Abdullatif.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano haya na matarajio yetu kuwa tutafanya vyema, tunatarajia kupata ushindani mkali kutoka kwa waogeleaji wa timu nyingine ambazo nazo zimejiandaa kwa ajili ya kupata ushindi,” anasema Alidina.

Mbali ya Bluefins, timu nyingine zitakazoshiriki katika mashindano hayo ni Dar Swim Club (DSC), Mwanza ,  Shule ya Kimataifa ya Geita Gold Mine, Champion Rise, Shule ya Kimataifa ya Moshi (ISM), Isamilo, Taliss na shule ya kimataifa ya wasichana ya  Loretto.