Huyu hapa mrithi wa Cannavaro

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti kwenye kambi ya Yanga mjini hapa, Cannavaro amesema kama atatangaza kustaafu kuitumikia klabu hiyo basi Ninja atahitaji mechi tano tu kali ili kumpa makali zaidi.

UMRI umemtupa mkono na sasa, nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameamua kutangaza mrithi wake kwenye kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara. Sasa Cannavaro amewaangalia mabeki wote ndani ya klabu yake kisha Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuwa, ndiye atakuwa mrithi wake.

Akizungumza na Mwanaspoti kwenye kambi ya Yanga mjini hapa, Cannavaro amesema kama atatangaza kustaafu kuitumikia klabu hiyo basi Ninja atahitaji mechi tano tu kali ili kumpa makali zaidi.

Amesema Ninja ana uwezo mkubwa wa kukaba na kuziba nafasi ya kupenyeza mipira na kwamba, ni moja ya mabeki wakatili wanaposimama katika beki ya kati.

Pia, alisema kocha wao aliyetimka George Lwandamina anahitaji pongezi kubwa kwa kuzalisha vipaji vipya ndani ya Yanga katika muda mfupi, ambayo jana ilifanya yake dhidi ya Welaytta Dicha mjini hapa.

“Kama nitastaafu leo basi kuna Ninja hapa Yanga kila kitu kitakuwa salama. Jamaa ni katili na anacheza soka tamu na ninamkubali kinoma. “Tunamuona mazoezini lakini wengine wanamuona kwenye mechi ni hatari sana na anaweza kufanya vitu ambavyo kila mmoja akashangaa. Ni jasiri na hapo Lwandamina anastahili pongezi kwa kuibua vipaji vipya,” alisema Cannavaro.