Mama Kanumba aibukia filamu Captain Habona

Monday April 9 2018

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Akiwa katika harakati za kutaka kufufua kampuni ya mwanae, marehemu Steven Kanumba, Flora mtegoa anatarajiwa kuonekana katika filamu mpya ya ‘Captain Habona’ aliyocheza kama nahodha wa meli.
Filamu hiyo inatarajiwa kutoka hivi karibuni, inayotayarishwa na kampuni ya ‘Kanumba The Great’, chini ya muongozaji wa filamu hiyo, Fredrick Michael, ambaye kitaaluma ni nahodha wa meli.
Michael aliiambia MCL Digital filamu hiyo imechezwa ndani ya meli ya siku nyingi ya MV Liemba yenye miaka zaidi ya 100, inayofanya safari zake katika ziwa Tanganyika.
Pamoja na waigizaji wengine, Michael alisema Mama Kanumba ameitendea haki nafasi ya unahodha wa meli ambaye yeye ni mmoja wa wahusika wakuu.
“Kwa kweli Mama Kanumba ni mtu anayejua sanaa na imekuwa rahisi katika kumuongoza na pia mmoja wa watu waliotoa ushauri wa kuifanya filamu yetu hii iwe nzuri, nina imani watu wataifurahia,”alisema muongozaji huyo.
Akielezea kwa ufupi hadithi iliyopo ndani ya filamu hiyo, alisema ni ya kijana mmoja aliyeishi maisha ya tabu baada ya kutelekezwa na baba yake ambapo baadaye anakuja kumpata na kuahidi kumlipia ada ya chuo.
“Lakini kwa bahati mbaya siku inapowadia na kumfuata alipo anakutana na mama yake wa kambo ambaye anamwambia baba huyo ameshafariki na baada ya kusota na kuja  kupata kazi ya unahodha katika meli hiyo ya Mv Liemba anajulishwa kuwa muuaji wa baba yake yupo ndani ya meli hiyo na kuanza kumsaka,”alisema Michael.