#WC2018: Sio kwa mpanio huu wa Russia!

Muktasari:

Ni lengo zuri, kwani Ufaransa ilipoandaa fainali hizo ilitwaa ubingwa jambo ambalo lilikuwa halijafanyika tangu miaka ya 70.

Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, Russia wamepania kufika nusu fainali katika michuano ya mwaka huu.

Ni lengo zuri, kwani Ufaransa ilipoandaa fainali hizo ilitwaa ubingwa jambo ambalo lilikuwa halijafanyika tangu miaka ya 70.

Russia imewahi kushiriki katika Fainali 10 tu za Kombe la Dunia, na mwaka huu inashiriki ikiwa mwandaaji wa fainali.

Russia iliwahi kushinda taji la kwanza la mashindano ya mabara mwaka 1960 ikiwa kama Umoja wa Kisovieti. Baada ya kuvunjika kwa Umoja huo (Urusi), Russia ilicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Mexico, Agosti 16, 1992 wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0, timu yao ikiundwa na wachezaji wa zamani kabla ya kuvunjika kwa Sovieti.

Haina historia nzuri na Kombe la Dunia, kwani tangu mwaka 1994 mpaka 2014 ilipoanza kushiriki huishia hatua za makundi pekee. Hatua kubwa kuwahi kuipiga katika mashindano ya kimataifa ni nusu fainali ya Mashindano ya Mataifa ya Ulaya (Euro 2008).

Russia ikiongozwa na kocha Pavel Sadryin kwa mara ya kwanza ilipangwa kundi namba 5 katika hatua za kufuzu Kombe la Dunia la mwaka 1994.

Ikiwa na timu za Ugiriki, Iceland, Hungary na Luxembourg, Russia ilishinda michezo sita na kutoka sare miwili na hivyo kufuzu.

Katika mashindano yenyewe ya Kombe la Dunia, Russia ilipangwa Kundi B na timu za Cameroon, Sweden na Brazil. Lilionekana kuwa kundi gumu kufuzu kwa Russia ikiwa na nafasi finyu baada ya kupoteza michezo miwili (dhidi ya Brazil na Sweden) na kisha kushusha mvua ya mabao 6-1 dhidi ya Cameroon. Russia iliaga mashindano kwa kuwa na pointi tatu na kocha wao alionyeshwa mlango wa kutokea.

Chini ya kocha mzawa Stanislav Cherchesov, Russia inakwenda katika Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 ikiwa ni mwenyeji.

Katika hatua za makundi ipo kundi A na timu za Saudi Arabia, Misri na Uruguay. Kundi hili Saudi Arabia ndio inaonekana kuwa kibonde, lakini kwa Misri mambo yatakuwa tofauti kwani, wamepania kufika mbali na kuweka historia kwenye michuano hiyo.