Kwa Ngoma, ubingwa ni wetu mapemaaa

Donald Ngoma

YANGA na Simba kwa sasa wanatambia kwelikweli huko mtaani. Lakini, kubwa ni mbio za ubingwa ambao kwa msimu huu ni lazima uangukie kwenye mtaa mmoja ama Msimbazi au Jangwani.

Huko Yanga baada ya kurejea kwa straika wake matata, Donald Ngoma ambaye aliyekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi, sasa morali imeongezeka na mashabiki wake wameanza kutamba.

Straika wa zamani wa Yanga, Henry Morris alisema kurejea kwa Ngoma kunaipa nafasi mabingwa hao watetezi kubeba taji hilo kama tu atakuwa kwenye kiwango kile kile.

“Chirwa yupo vizuri na kama Ngoma naye atarudi tena akiwa na kiwango kile kile, basi pale mbele itakuwa hapatoshi kwa sababu wote ni wapambanaji,” alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa klabu hiyo, Hussein Nyika, alisema mchezaji huyo anarejea katika mazoezi ya pamoja leo Alhamisi.

“Ngoma alikuwa akifanya mazoezi ya peke yake, lakini taarifa kutoka kwa daktari ni kuwa, anajiunga katika mazoezi ya pamoja na wenzake kujiandaa na mchezo wa watani Simba,” alisema.