Chelsea yaibania Man United

London, England. Manchester United imekwaa kisiki kupata saini ya mchezaji nyota wa Chelsea Willian katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, alisema kuwa hana mpango wa kutimka Chelsea na amewataka mashabiki wa klabu hiyo kumuunga mkono.

Man United ilikuwa na matumaini ya kupata saini ya mchezaji huyo ili kwenda kuimarisha kikosi hicho.

Jose Mourinho alirusha ndoano akidai Willian ni mchezaji bora mwenye sifa za kucheza Man United.

William anayetamba katika kikosi cha kwanza kwa Mtaliano Antonio Conte, alisema hana mpango wa kuhama Chelsea na amewataka mashabiki wa klabu hiku kumsapoti.

Awali, ziliibuka tetesi kuwa mchezaji huyo amekubali kutua Old Trafford katika dirisha dogo kabla ya kujitokeza hadharani kukana taarifa hiyo.

“Siku zote nimekuwa na furaha Chelsea. Naipenda sana klabu hii kwa roho moja, siwezi kuondoka naomba mashabiki watulie wanipe ushirikiano,” alisema Willian.

Willian mwenye miaka 29, alifunga bao la kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu England walioshinda mabao 3-1 dhidi ya Huddersfield.