Simba ina zali na vibabu

SIMBA iko mbioni kumsajili straika Mzambia, Jonas Sakuwaha, ambaye ameonyesha kiwango cha kuvutia kwenye majaribio ikiwemo kufunga bao murua dhidi ya KMC Ijumaa iliyopita, lakini umri wa nyota huyo umeibua zogo.

Sakuwaha ana miaka 34 hivyo kuzua hofu kuwa huenda Simba itaingia mkenge kwa kusajili mchezaji ‘babu’ ambaye atashindwa kuendana na kasi ya Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo tathmini ya Mwanaspoti inaonyesha kuwa nyota wengi wenye umri mkubwa walipotua Simba walifanya vizuri.

Mchezaji wa kwanza ni kipa Ivo Mapunda ambaye Simba walimsajili mwaka 2013 ambapo kwa mujibu wa mtandao wa Football alikuwa na miaka 36.

Ivo ambaye alionekana kiwango kimeisha baada ya kuchezea timu kama Prisons, Yanga, St. George, Congo United, AFC Leopards na Gor Mahia, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha idara ya kipa ambayo ilionekana tatizo kubwa kwa Simba tangu ilipoachana na Juma Kaseja.

Nyota mwingine ambaye Simba iliwahi kumsajili akiwa na umri mkubwa ni Mzimbabwe, Justice Majabvi ambaye alitua akiwa na umri wa miaka 33.

Majabvi anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji, alifanikiwa kuwa muhimili imara wa Simba na hata alipoondoka baada ya kumalizika kwa msimu wa 2015/2016, mashabiki wengi wa Simba hawakufurahishwa na uamuzi wake licha ya hapo awali kuwapa wasiwasi.

Msimu uliopita, Simba iliwasajili mabeki Method Mwanjali aliyekuwa na umri wa miaka 32 ya soka pamoja na beki wa zamani wa TP Mazembe na Esperance, Janvier Bokungu aliyekuwa na miaka 29 ya soka ambao wote waliiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi pamoja na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA.