Yanga kumfunga Chirwa

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo Mzambia ameanza msimu huu vizuri na tayari amefunga mabao sita katika Ligi Kuu Bara msimu huu

Yanga imekubaliana kwa kauli moja kwamba mshambuliaji Obrey Chirwa lazima apewe mkataba mpya haraka mno.

Vigogo wa Jangwani, wanakuna kichwa kupata mashine nyingine ya maana ili kumpiga chini mshambuliaji anayewaletea nyodo Donald Ngoma, lakini kocha George Lwandamina amewaambia inyeshe au liwake lazima wambakize Chirwa.

Mpango huo wa kumpa ulaji Chirwa umetokana na kiwango bora alichoonyesha siku za karibuni, lakini kilichowavutia zaidi ni kubadilika kwa nidhamu yake na hamasa anayowapa wenzie katika siku za karibuni.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Yanga iliyochini ya Mwenyekiti Hussein Nyika na Makamu wake Mustapha Ulungo ni kwamba vigogo hao wameanza kupeana majukumu ya kukamilisha mkataba huo wa Chirwa haraka ikiwa ni njia ya kujiondolea presha.

Chirwa anamaliza mkataba wake Julai mwakani lakini Yanga hawataki kuingia katika Ligi ya Mabingwa Afrika,mshambuliaji huyo mwenye mabao sita akiwa hajamwaga wino wa kubaki katika timu hiyo.

Wamemkabidhi Lwandamina jukumu la kumlainisha Chirwa ili mpango huo ukamilike kazi ambayo imeanza tayari.

Akithibitisha hilo Ulungo ambaye ni nadra kuzungumza na magazeti alisema kwa kifupi:"Tunaheshimu nguvu ya kila mchezaji na mmoja wao ni Chirwa amekuwa na kiwango bora sio tu msimu huu lakini hata msimu uliopita,namsubiri mwenyekiti wangu tuanze jukumu hilo la kumalizana naye tunahitaji abaki hapa zaidi hilo halina mjadala."