Mrundi wa Simba atakayeanza na Yanga atua Dar

Djuma Masudi

Muktasari:

Djuma Masudi ndiye anayekuja kuchukua nafasi yake na huenda akaiwahi mechi dhidi ya Yanga Oktoba 28 kwenye Uwanja wa Taifa.

Mrithi wa aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ametua leo jijini Dar es Salaam.

Djuma Masudi ndiye anayekuja kuchukua nafasi yake na huenda akaiwahi mechi dhidi ya Yanga Oktoba 28 kwenye Uwanja wa Taifa.

Kama humfahamu Djuma enzi zake za uchezaji alikuwa straika wa Inter FC ya Ligi Kuu ya Burundi. Ni kocha kijana mwenye mizuka na uwezo mkubwa wa kupandisha morali ya wachezaji kama alivyo Jamhuri Kihwelu 'Julio' au Ettiene Ndayiragige wa Mbao FC.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka la Rwanda, Djuma ni kocha  mwenye maneno mengi na rafiki wa wachezaji na inapotokea timu imeshinda hupandisha wazimu kama kocha wa Chelsea, Antonio Kante.

Kocha huyo ameipa Rayon Sports ya Rwanda ubingwa msimu uliopita kabla ya kuachia ngazi. Mafanikio yake  katika Ligi ya Rwanda msimu uliopita yameivutia Simba na kuona ni mtu sahihi wa kumsaidia kocha wa sasa Joseph Omog.

Mmoja wa mabosi wa juu wa Simba aliliambia Mwanaspoti.com kuwa wamevutiwa na kocha huyo na tayari wamefanya naye mazungumzo ili aje kuziba nafasi ya Mayanja ambaye anaachana na timu hiyo baada ya kufanya kazi kwa miezi 22.