Beki Singida Utd ampiku Ajib

Dar es Salaam.BEKI wa Singida United, Shafik Batambuze amefanikiwa kunyakua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Septemba katika Ligi Kuu Bara kwa kumzidi ujanja Ibrahim Ajib wa Yanga na Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar.

Batambuze anayecheza beki ya pembeni  ameteuliwa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali vya ligi hiyo.

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida kupata pointi 10 katika michezo minne iliyocheza ndani ya mwezi huo na kuisaidia timu yake kutoka nafasi ya 10 hadi ya nne iliyopo sasa.

Singida ndiyo iliyokusanya alama nyingi kwa mwezi huo ukilinganisha na timu nyingine 15 zinazoshiriki VPL kwani iliifunga Mbao FC mabao 2-1 mjini Dodoma, ikaichapa Stand United bao 1-0 mjini Shinyanga na kuilaza Kagera Sugar bao 1-0 mjini Dodoma kabla ya kulazimisha sare ya 1-1 na Azam mjini humo.

Michezo yote hiyo Batambuze alicheza dakika zote 90 kwa kila mchezo, ambayo ni sawa na kucheza dakika 360.

Ajibu alitoa mchango mkubwa kwa Yanga uliowezesha kupata pointi nane kwa mwezi huo, baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili, ambapo pia Mohammed Issa aliisaidia timu yake kupata pointi nane katika michezo minne kwa mwezi huo, ikishinda miwili na kutoka sare miwili.

Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazawadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali. Batambuze atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.