Mipango ya Yahya si mchezo

MWENYEKITI wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Hamad Yahya ameamua kupambana kutetea nafasi yake ya uongozi katika bodi hiyo yenye mamlaka ya kusimamia ligi zote kubwa nchini.

Uchaguzi wa bodi hiyo utafanyika Jumapili ya wiki hii chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo mwenyekiti wake ni Wakili Msomi, Revocatus Kuuli ambaye alisimamia uchaguzi uliopita wa TFF.

Yahya analazimika kupambana na hali yake kuchuana na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ambaye ameamua kujitosa kumpa upinzani.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Yahya anaeleza namna walivyofanikiwa katika awamu ya kwanza ya uongozi na vitu alivyopanga kufanya akichaguliwa awamu ya pili.

“Nataka bodi ya ligi iwe kampuni inayojitegemea. Tumefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita na sasa tunahitaji kujitegemea,” anasema Yahya.

“Kumekuwa na mwingiliano katika mamlaka ya Bodi ya Ligi. Mfano sasa bodi haina mamlaka kamili ya kuingia mikataba kwani tuko chini ya TFF. Hatuwezi pia kufanya biashara kwani tunabanwa na kanuni.

“Pia, tulipata changamoto katika uongozi uliopita wa TFF kwani uliingilia baadhi ya mambo kama Ratiba ya Ligi Kuu kwa kuipangua mara kwa mara bila kutushirikisha. Tunashukuru sasa tunakwenda sawa na uongozi mpya,” anaeleza.

“Tunataka bodi sasa iwe na mamlaka kamili ya kusimamia Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili. TFF ijikite zaidi katika utawala na maendeleo ya soka kwa jumla.”

HALI YA BODI

“Nimekuwepo kwenye bodi tangu imeanza, tulikuwa na changamoto nyingi mwanzo lakini sasa tumefikia hatua nzuri, mwanga unaonekana huko mbele,” anasema Yahya.

“Mfano mwanzo fedha za udhamini zilikuwa zinalipwa moja kwa moja kwa klabu na changamoto zilikuwa nyingi. Kuna timu kama Azam na Mtibwa Sugar zinadai fedha zao za zawadi za miaka saba nyuma.

“Kwa sasa klabu zinalipwa kwa wakati. Tulibadili mfumo na fedha zikawa zinapita bodi kisha tunazilipa klabu, angalau imetatua matatizo,” anaeleza.

UDHAMINI NA MAPATO

Yahya anasema miongoni mwa changamoto zilizopo mbele yao ni kupatikana kwa wadhamini zaidi katika Ligi Kuu pamoja na ligi za chini.

“Mkataba wa sasa wa Vodacom unamalizika, kama nitachaguliwa tutaanza mchakato mapema sana ndani ya mwezi huu. Ligi yetu ina thamani kubwa zaidi ya fedha tunayopata sasa (Sh2.5 kwa mwaka), tunahitaji zaidi.

“Kwa sasa tumetafuta kampuni kwa ajili ya kututafutia wadhamini, tunatamani kuona udhamini wa klabu unaongezeka angalau timu zipate nafuu katika soka lao,” anasema mkurugenzi huyo wa Kagera Sugar.

“Chaganmoto nyingine katika mfumo wa kielektroniki, mapato yameshuka. Tuliwahi kuingiza Sh600 milioni kwenye mechi ya Simba na Yanga, lakini sasa tunapata fedha kidogo sana. Tunahitaji mfumo mpya.

“Tumebadili pia kanuni na kumpa mwenyeji asilimia 40 ya mapato ya mechi. Tunafikiria pia hapo baadaye mapato yote yaende kwa mwenyeji, ili kumfanya aitangaze mechi na kuhamasisha watu waende uwanjani,” anasema Yahya.

CHANGAMOTO

“Tumekuwa na changamoto ya ubovu wa viwanja na pia kuingiliana kwa ratiba ya viwanja. Tumepanga kuwa na kikao na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaomiliki viwanja vingi vinavyotumiwa kwa ligi, Oktoba 20, kuangalia namna ya kuviboresha viwanja hivi.

“Pia, Changamoto ipo katika upangaji wa ratiba. Klabu hazina fedha hivyo tunapanga kwa kuangalia namna ya kuwapa unafuu katika safari zao za mikoani. Ingekuwa hakuna tatizo hilo ratiba ingetulia.”

“Kwa upande wa adhabu ni kweli baadhi zinachelewa kwa kuwa bodi tunaruhusiwa tu kumsimamisha mtu na kusubiri kamati zimwajibishe. Kama bodi itakuwa huru tunaweza kuwa na maamuzi zaidi.

“Kwa sasa tunajitahidi kugharamia vikao vya baadhi ya kamati ili angalau vikae na kutoa maamuzi kwa wakati, hili linaweza kupunguza malalamiko,” anasema.

Yahya anakiri Ligi Daraja la Kwanza haina udhamini, usalama na ufuatiliaji mdogo.

“Viwanja vingi havina usalama wa kutosha. Kuna matukio mengi yanatokea inakuwa ni ngumu kuyadhibiti. Usalama pia umekuwa umekuwa changamoto.”

MIPANGO YAKE

Bosi huyo wa Kagera Sugar anasema mipango yake ni Bodi ya Ligi inakuwa huru pamoja na kutafuta udhamini zaidi kwa ligi na timu za Ligi Kuu.

“Natamani kuona kunakuwepo kwa umoja na mshikamamo miongoni mwa klabu. Tuwe na msisitizo katika soka la vijana. Mfano sasa kanuni inasema timu mwenyeji inapocheza lazima timu yake ya vijana itafute mchezo wa kucheza kama utangulizi, lazima tusimamie hilo.

“Nimepanga pia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika Bodi ya Ligi ili kuongeza weledi. Utunzaji wa kumbukumbu pia umeimarishwa, tunataka kwenda kisasa. Udhamini pia unatakiwa kuongezwa timu za Ligi Kuu pamoja na ligi tunazozisimamia. Bodi pia iwe huru na ijitegemee,” anaeleza.