Wamebugi

Thursday October 12 2017

 

MOSCOWRUSSIA. NANI kaenda, nani kabaki kwenye mchakamchaka wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazotimka mwakani imeshafika mwisho. Sasa inajulikana dhahiri mastaa wangapi wametoboa na wangapi wameshindwa.

Hii hapa ni orodha ya mastaa unaowaaminia, lakini hawatakuwapo kwenye fainali hizo zitakazofanyika huko Russia mwakani. Hii ni baada ya kushindwa kufuzu na timu zao za taifa licha ya ubora walionao.

PIERRE-EMERICK

AUBAMEYANG

Staa wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, alikaribia kuisaidia Gabon kuweka historia ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, lakini walishindwa kukamilisha ndoto hizo.

Aubameyang hakuonyesha makali ya kufunga mabao katika raundi ya tatu, lakini akiwa na umri wa miaka 28 bado ana nafasi ya kusubiri fainali nyingine za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika miaka minne ijayo.

GARETH BALE

Shujaa wa Wales aliyewafanya wafike nusu fainali za Euro 2016, Gareth Bale, ameshindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Maumivu ya nyonga yalimfanya Bale awe nje ya uwanja Jumatatu wakati Wales ilipocheza mechi muhimu dhidi ya Jamhuri ya Ireland ikihitaji sare tu kufuzu, lakini ikachapwa bao 1-0 na hivyo kupoteza tiketi.

EDIN DZEKO

Kiwango bora cha Ubelgiji kwenye Kundi H, kiliziacha Ugiriki na Bosnia & Herzegovina kuishia kupigania nafasi ya pili, mchuano ulioshuhudia Ugiriki ikiibuka washindi.

Kwa maana hiyo, Bosnia yenye staa kama Edin Dzeko haitakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia licha ya kwamba alipambana na kufunga mabao matano kwenye mechi za kufuzu. Ndio maana staa huyo wa AS Roma naye hatakwenda Russia.

MAREK HAMSIK

Baada ya kuanza vibaya katika mechi zake za kwanza za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa kukumbana na vichapo viwili, Marek Hamsik, aliisaidia Slovakia kuendeleza mapambano hadi dakika za mwisho.

Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Malta kwenye mechi za siku ya mwisho uliifanya kushika namba mbili Kundi F nyuma ya England, lakini kutokana na matokeo ya makundi mengine, wameikosa tiketi ya wapili bora.

RIYAD MAHREZ

Hakutakuwa na fainali za Kombe la Dunia kwa supastaa wa Leicester City na Algeria, Riyad Mahrez. Staa huyo, ambaye misimu miwili iliyopita alikuwa bora kabisa akinyakua tuzo ya ubora ya Afrika, safari hii ameshindwa kufanya kitu cha maana katika kikosi chake cha Algeria.

Mahrez ameshindwa kufurukuta mbele ya Nigeria, Zambia na Cameroon.

ARJEN ROBBEN

Alifika fainali na Uholanzi yake mwaka 2010 na pia nusu fainali 2014, kumbe ndio zilikuwa fainali zake za mwisho za Kombe la Dunia kwani safari hii Arjen Robben na kikosi chake wameshindwa kufuzu.

Robben ameamua kustaafu soka la kimataifa muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Sweden, ambapo alifunga mara mbili kwenye ushindi wa 2-0.

ALEXIS SANCHEZ

Baada ya kuing’arisha Chile kushinda mara mbili mfululizo Copa America mwaka 2015 na 2016 na licha ya kufunga mabao saba, supastaa Alexis Sanchez, ameshindwa kuisaidia timu yake kukamatia tiketi ya Kombe la Dunia la mwakani.

Kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brazil katika mechi yao ya mwisho, kimewafanya kuporomoka hadi nafasi ya sita katika msimamo wa Amerika Kusini.

ARTURO VIDAL

Sanchez si staa pekee wa Chile atakayekosekana Kombe la Dunia mwakani. Mwingine ni kiungo mpambanaji, Arturo Vidal.

Kiungo huyo alifunga mabao sita katika mechi za kufuzu, lakini jambo hilo halikusaidia kuinusuru timu yake. Ni mara ya kwanza tangu mwaka 2006, Chile kushindwa kufuzu Kombe la Dunia.