Ebwanaee huyu Niyonzima

Muktasari:

Azam ndiyo inaoongoza kwani inalipa kiasi kinachofikia Sh160 milioni licha ya kwamba imepunguza matumizi yasiyo ya lazima msimu huu.

KUNA taarifa nzuri Msimbazi. Siyo ile ya kuongezeka idadi ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wala kuongoza Ligi Kuu Bara (VPL). Simba imejiimarisha kifedha kwa sasa na kushika nafasi ya pili ambapo mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi kwa mwezi inafikia Sh130 milioni.

Azam ndiyo inaoongoza kwani inalipa kiasi kinachofikia Sh160 milioni licha ya kwamba imepunguza matumizi yasiyo ya lazima msimu huu.

Mnyama Simba anapewa jeuri na bilionea, Mohammed Dewji, ambaye ameamua kuingia na miguu yote kuhakikisha timu inafanya vizuri, gharama za Simba zimeimarika kutokana na usajili mpya uliosheheni mastaa wakubwa, lakini uongozi ulikuwa imara kwenye maelewano.

Msimu uliopita Simba ilikuwa ikilipa Sh80 milioni kwa mwezi. Yanga ambayo ni mabingwa wa mara tatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara, msimu uliopita walikuwa juu, wameporomoka hadi nafasi ya tatu ambapo sasa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi kwa mwezi inafikia Sh115 milioni tu.

Sababu kubwa ambayo imetajwa kuishusha Yanga ni kuondoka kwa nyota wake wawili, Vincent Bossou ambaye bado nafasi yake iko wazi na Haruna Niyonzima ambaye nafasi yake imezibwa na Papy Kabamba Tshishimbi anayetumia gharama za wastani.

Niyonzima noma

Katika orodha ya wachezaji wa Simba, Yanga na Azam inaonekana Niyonzima ndiye aliyefanya maelewano ya kijanja zaidi msimu huu kuanzia kwenye usajili mpaka mshahara. Amewazidi wote.

Kiungo huyo Mnyarwanda anakinga dola 4,000 (Sh 8.8 milioni) kwa mwezi.

Niyonzima alikamilisha uhamisho wake kwenda Simba Julai mwaka huu baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka sita na kushinda mataji manne ya Ligi Kuu Bara.

Niyonzima anafuatiwa kwa karibu na Mganda Emmanuel Okwi wa Simba anayepokea kiasi cha Sh8.2 milioni kwa mwezi na Mzimbabwe Donald Ngoma wa Yanga anayechukua dola 3,500 (Sh7.7 milioni).

Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini pia kwamba Mzimbabwe Thabani Kamusoko, Mzambia Obrey Chirwa na Mrundi Amissi Tambwe nao ni miongoni mwa wanaolipwa fedha ndefu nchini ambapo wanachukua dola 3,000 (Sh6.6 milioni) kila mmoja.

Kwa upande wa wachezaji wazawa, uchunguzi umebaini kuwa John Bocco wa Simba ndiye kinara akiwa bado yupo juu kwa mshahara wake wa sasa wa Sh6.9 milioni, ikiwa ni zaidi ya fedha alizokuwa akilipwa wakati akiwa Azam ambao wanaamini atarudi Chamazi baada ya mkataba wake kumalizika Msimbazi.

Mkongomani Kabamba Tshishimbi aliyetua Yanga akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland, analipwa dola 2,500 (Sh5.5 milioni) sawa na straika Mghana wa Simba, Nicholas Gyan.

Azam nako

Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini kuwa malipo ya wachezaji na benchi la ufundi yameshuka hadi Sh160 milioni kwa mwezi. Hata hivyo licha ya Azam kuwa kinara cha kuwalipa nyota wake, lakini malipo hayo yameshuka kwa kiwango kikubwa kwani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita uchunguzi unaonyesha walikuwa wakilipa zaidi ya Sh300 milioni kwa mwezi mmoja.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdul Mohammed alinukuliwa na Mwanaspoti akisema: “Wakati nafika hapa matumizi ya klabu yalikuwa juu sana. Wakati mwingine yalifika zaidi ya Sh500 milioni kwa mwezi, ni fedha nyingi sana.

“Mishahara ilikuwa juu, lakini sasa angalau imeshuka kwa asilimia 48. Matumizi mengine pia yamepungua, hii inasaidia kuendana na hali halisi ya klabu pamoja na uchumi wa nchi.”

Mwanaspoti linajua kuna wachezaji wa kigeni wa Azam walikuwa wakilipwa hadi dola 7,000(Sh15. 5milioni), lakini uchunguzi wetu umebaini kwa sasa mchezaji wa juu klabuni hapo analipwa dola 3,000 (Sh6.6 milioni) tu.