RT yathibitisha kutopeleka timu mbio za dunia ila ni wanariadha wawili tu

Muktasari:

Wanariadha 12 walifikia viwango vya kushiriki mbio za dunia za vijana baada ya kufanya vizuri na kutwaa medali za dhahabu kwenye mashindano ya Afrika ya Kanda ya Tano yaliyofanyika Machi jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Shirikisho la riadha Tanzania (RT) limewaengua wanariadha 10 kushiriki mashindano ya dunia ya vijana yatakayoanza Julai 12 nchini Kenya.

Wanariadha 12 walifikia viwango vya kushiriki mbio za dunia za vijana baada ya kufanya vizuri na kutwaa medali za dhahabu kwenye mashindano ya Afrika ya Kanda ya Tano yaliyofanyika Machi jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelim Gidabuday alisema tayari wamethibitisha kutowapeleka wanaridha 10 kati ya 12 waliofuzu kwenye mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la riadha la Kimataifa (IAAF).

"Jana 'Juzi' ndiyo ilikuwa mwisho wa kuthibitisha ushiriki wetu IAAF, hatukuwa na namna zaidi ya kupeleka majina mawili kati ya 12 ya wanariadha wetu waliofuzu, ambao hao wawili watagharamiwa na IAAF,'' alisema Gidabuday.

Wanariadha wawili watakaoiwakilisha nchi ni Shomari Mtalimu na Winfrida Makenji ambao kwa mujibu wa Gidabuday hawataingia kambini zaidi ya kuandaliwa mazoezi maalumu kabla ya kuondoka nchini Julai 10.