Njombe Mji hawataki kukurupuka kusajili wachezaji majina pasipo viwango

Muktasari:

Mapema Mei mwaka huu klabu hiyo ilitangaza usaili wa wachezaji wenye sifa ya kuitumikia klabu hiyo  ambapo walijitokeza zaidi ya wachezaji 300, lakini walichujwa na kubaki ni wachezaji 27 pekee ambao wanaendelea mchunjo.

Mbeya. Klabu ya Njombe Mji FC itakayoshiriki Ligi Kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza imesema haisajili wachezaji kwa kukurupuka ili kuwa na kikosi bora kitakacholeta ushindani.

Mapema Mei mwaka huu klabu hiyo ilitangaza usaili wa wachezaji wenye sifa ya kuitumikia klabu hiyo  ambapo walijitokeza zaidi ya wachezaji 300, lakini walichujwa na kubaki ni wachezaji 27 pekee ambao wanaendelea mchunjo.

Msemaji wa Njombe Mji, Solanus  Mhagama alisema hadi sasa hakuna mchezaji aliyepewa mkataba wa kudumu.

Alisema kati ya wachezaji hao 27 wapo wengine 10 walioipandisha timu, lakini na wao hawajasaini mikataba kutokana na mahitaji ya Kocha Mkuu Hassan Banyai kutaka wachezaji wenye viwango vya uhakika.

‘’Hatutaki kusainisha mikataba mapema tukaingia ‘mkenge’ kutokana na ukweli kwamba tukitulia tutapata wachezaji wenye viwango kuliko kusajili wachezaji majina kwa kuiga wanavyofanya wenzetu,’’ alisema Mhagama.